
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, ametuma salamu za heri kwa klabu zote za Tanzania zinazoshiriki mashindano ya kimataifa barani Afrika.
Kwa niaba ya Serikali, Msigwa amesema anawatakia kila la kheri Simba SC, Yanga SC, Azam FC pamoja na Singida Black Stars ambazo zinashuka dimbani leo na siku zijazo kupeperusha bendera ya Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.
Aidha, Msigwa amekumbusha kuwa mpango wa Serikali wa “Goli la Mama” unaendelea kama ulivyoahidiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo zawadi hutolewa kwa kila goli la ushindi:
Hatua za awali: Shilingi milioni 5 kwa kila goli la ushindi
Robo Fainali: Shilingi milioni 10 kwa kila goli la ushindi
Nusu Fainali: Shilingi milioni 20 kwa kila goli la ushindi
Fainali: Zawadi maalum itaandaliwa, huku ushindi wa penati ukihesabiwa kama goli moja
Msigwa alisema:
“Ninatambua kuwa Yanga leo itacheza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Wiliete nchini Angola, Simba dhidi ya Gaborone ya Botswana, Azam nchini Sudan dhidi ya El-Merriekh na Singida Black Stars dhidi ya Rayon Sports kule Rwanda. Tunawatakia kila la kheri, na goli la mama lipo pale pale kuanzia hatua hizi za awali.”
Kauli hiyo imepokelewa kwa shangwe na mashabiki wa soka nchini, wengi wakiamini motisha hiyo itaongeza hamasa kwa wachezaji kufanya vizuri uwanjani na kuleta matokeo chanya.