Wakazi wa mtaa wa Maendeleo Mbweni, jijini Dar es Salaam wamekabidhi mahitaji mbalimbali katika kituo cha kulelea watoto cha Furaha kilichopo Mbweni Mpiji yenye thamani ya Shilingi 3,925,000.
Wakikabidhi mahitaji hayo mapema leo Septemba 20, 2025 Mwenyekiti wa Mtaa wa Maendeleo Bw. Salumu Yusuf amesema imekuwa ni desturi kwa wakazi wa mtaa huo kutoa sadaka ya shukrani kila mwaka kwa wahitaji katika maeneo mbalimbali.
Amesema mahitaji hayo ni pamoja na sabuni, sukari, mafuta, chumvi, unga,maharage mchele ,Tambi, Mafuta ya kupikia nyama ya kuku,sabuni za kufulia na za kufanyia usafi.
Tukio hilo lilitanguliwa na tukio muhimu la wakazi wa mtaa huo kupata kifungua kinywa na watoto hao ikiwa ni pamoja na kuwapa zawadi mbalimbali kama alama ya upendo.
Kwa upande wake Mlezi wa kituo hicho Sister Martha Massawe ameshukuru kwa upendo uliooneshwa kwa wakazi hao kwa kuwakumbuka wahitaji na kuwaomba waendelee na moyo huo wa upendo.
Amesema kuwa kwa sasa kituo hicho kilichopo ndani ya kanisa Kanisa katoliki kina jumla ya watoto 70 wanaolelewa kituoni hapo ambao wameletwa kutoka sehemu mbalimbali walikokuwa wakiishi katika mazingira magumu.