*Azungumzia kuhusu kutatua changamoto ya uhaba wa maji, agusia miundombinu ya barabara
Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Ruvuma
MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM)Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ameahidi Serikali katika miaka mitano ijayo itaendelea kutoa ruzuku ya pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea ya ruzuku sambamba na kutafuta masoko ya mazao ili wakulima wanufaike na jasho lao.
Pia ameahidi kuwa katika miaka mitano ijayo Serikali atakayoiunda baada ya kupata ridhaa ya wananchi wataendelea kukamilisha miradi ya maendeleo huku akisisitiza kuendelea kutatua changamoto ya uhaba wa maji kwa kukamilisha miradi ya maji katika maeneo mbalimbali.
Akihutubia maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma ikiwa ni mkutano wake wa kwanza katika Mkoa huo,Mgombea Dk.Samia ametumia nafasi hiyo kuwapongeza wananchi wa Mbinga kwani wamefanya vizuri katika kilimo.
“Niwapongeze kwasababu kwa Wilaya mmeongeza uzalishaji wa mazao ha chakula lakini na mazao ya biashara.Niwaahidi serikali yenu itaendelea kutoa ruzuku kwa pembejeo ,mbolea na pembejeo zingine
“Kwa wafugaji pia tutaendelea kutoa ruzuku ya chanjo pamoja na kuendelea kutoa huduma za ugani.Ahadi yangu kwenu serikali tutakayoiunda itaimarisha masoko ya mazao yetu ya kuendelea kutafuta bei nzuri kwa ajili ya mazao yetu ili mkulima afaidike na nguvu zake ,mkulima afaidike na jasho lake.Hiyo ndio ahadi yangu kwenu.”
Pamoja na hayo Dk.Samia amesema amefika katika Wilaya ya Mbinga kuomba kura ili kuendelea kufanya ile kazi ambayo wameianza miaka mitano iliyopita.
“Nimekuja kwa kujiamiani na ujasiri mkubwa kwasababu miaka mitano iliyopita tumeweza na mitano inayokuja kwa uwezo wa Mungu tutaweza.Katika afya ,elimu,umeme na maji tunakwenda kukamilisha miradi yote
“Uzuri ni kwamba tulitekeleza zaidi ya Ilani ilivyoelekeza hasa kwenye afya,elimu na maji tumetekeleza zaidi.Umeme tuliambiwa vijijini sasa tuko katika vitongoji na ukweli tumeshaunganisha nusu ya vitongoji vya Tanzania tayari vina umeme.Miaka mitano ijayo tunakwenda kumaliza nusu iliyobakia ili kila mtanzania awe amepata umeme.”
Kuhusu maji,Dk.Samia amesema ukiangalia kitaifa Serikali upatikanaji wa maji inakaribia asilimia 90 lakini kimkoa bado kuna mikoa iko nyuma hivyo Serikali ina kazi ya kufanya kumalizia miradi ya maji.
Ameongeza kuna maeneo bado hayajapata maji akitolea mfano katika Wilaya ya Mbinga kuna miradi ya maji hivyo ikikamilika wanakwenda kumaliza changamoto ya uhaba wa maji na kila mwanambinga atapata maji
Aidha amesema katika masuala ya afya ,elimu na huduma nyingine muhimu za kijamii zitaendelea kutekelezwa na kila awamu inayokuja kwani Watanzania wanazaa na kwasababu watoto wanakuwa hivyo na mahitaji nayo yataendelea kukua.
Kwa upande wa miundombinu ya barabara,Mgombea Urais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema Serikali katika mitano ikayo itaendelea kutekeleza miradi ya Ujenzi wa barabara kwa kumaliza zile ambazo ujenzi unaendelea.
“Kuna barabara ambazo tumezitaja katika Ilani ya uchaguzi 2025-2030 ambazo a inakwenda kujengwa. Zipo barabara zitakazojengwa kwa kiwango cha lami na kiwango cha changarawe ili zipitike mwaka mzima iwe jua iwe mvua.
“Pia tutaendelea kujenga madaraja yale ambayo yanakatisha mawasiliano baina ya pande mbalimbali na kwa wilaya ya Mbinga utakwenda kujenga lile daraja la maalum la mto Lumeme ,kwahiyo kuhusu barabara tutaendelea.
“Ndugu zangu hakuna mradi ghali kama miradi ya ujenzi wa barabara kwani kilometa moja ya barabara ni ujenzi wa vituo viwili vya afya na ndio maana hatuendi kwa kasi sana ila tukipunguza mzigo wa Ujenzi wa afya,shule ,maji tutakwenda haraka zaidi katika kujenga barabara
Pia amezungumza kuhusu kauli mbiu ya CCM katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu unaokwenda kufanyika Oktoba 29 ambayo inasema Kazi na Utu Tunasonga Mbele.
“Mkitupa ridhaa yenu ya kuendelea kuongoza Serikali sisi tutakwenda kufanyakazi pamoja nanyi ili tunyanyue utu wa mtanzania ,utu wa mwana Mbinga ,utu wa mwana Ruvuma na utu wa kila mmoja bila kujali dini ,kabila wala rangi .
“Ndio maana Serikali yetu tunamimina fedha nyingi katika miradi ya maendeleo ili tuweze kunyanyua utu wa mtu.”