*Aahidi kujenga viwanda vya kuongeza thamani ili kuongeza ajira kwa vijana
Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Ruvuma
MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)Dk. Samia Suluhu Hassan amesema katika Mkoa wa Ruvuma katika miaka mitano iliyopita Serikalini imetekeleza kwa kiasi kikubwa miradi ya maendeleo ya kijamii katika sekta za maji, elimu, afya na umeme serikali imetekeleza miradi hiyo kwa kasi kubwa.
Akizungumza na wananchi wq Songea Mjini katika Uwanja wa VETA mkoani Ruvuma Dk.Samia ameeleza hatua kwa hatua maendeleo ambayo yamepatikana ndani ya Mkoa huo kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita .
Kuhusu maji amesema kuna miradi mingi ambayo inaendelea kutekelezwa ndani ya mkoa huo na itakapokamilika itapita kiwango cha upatikanaji maji kilichoelekezwa na ilani ya uchaguzi (2020 – 2025).
“Kwa hiyo bado miradi inaendelea, maji yatapatikana niwaombe tuwe wastahimilivu ili wakandarasi wafanyekazi zao vizuri na maji yapatikane,” alibainisha.
Kwa upande wa elimu Dk.Samia amesema kwamba ujenzi wa madarasa, shule mpya umefanyika huku serikali ikiendelea kutoa elimu bila malipo.
Pia, amegusia ujenzi wa Chuo Kikuu cha Uhasibu Arusha tawi la Songea ambapo ameeleza kwamba chuo hicho kitakamilika kitachukua wanafunzi 10,000 kwa mkupuo.
“Ni fursa nzuri kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kuhamasika kusoma fani mbalimbali zitakazotolewa chuoni hapo.Najua tutakuwa na Wahasibu wengi kutoka Ruvuma kutokana na uwepo wa Chuo hiki.”
Dk.Samia pia amesema serikali itatekeleza ujenzi wa chuo cha wenyeulemavu eneo la Liganga jimbo la Peramiho kitakachoweza kutoa mafunzo yaliyokusudiwa.
Kuhusu mkakati wa nishati safi, ameeleza kwamba Serikali imetekeleza mkakati huo zaidi ya ilivyotarajiwa katika ilani.
“Ilani ilituambia tukifika 2025 vijiji vyote viwe na umeme lakini serikali ipo katika vitongoji kuunganisha umeme. Takriban vitongoji nusu vya Tanzania tayari vimeshaunganishwa umeme.
“Lakini tunafanya hivyo kwa sababu tuliahidi kila wilaya kuwa na kongani za viwanda na tunataka tutakapoanza kuweka kongani za viwanda, umeme uwe umeshafika na ndiyo maana tunakwenda kwa kasi.”
Ametoa mfano Mabada serikali itaweka viwanda vya kuongeza thamani zao la misitu ili kuongeza ajira na kukuza uchumi kwa vijana na Taifa.
Dk. Samia amesema uwepo wa umeme kutavutia wawekezaji wengi zaidi kuwekeza katika maeneo hayo.
Ameongeza kuwa serikali inakusudia kuweka viwanda vya kuongeza thamani zao la kahawa na parachichi.
“Kule Peramiho tumepata mwekezaji mkubwa wa kiwanda cha sukari na shamba kubwa la miwa. Hii pia ni fursa nyingine kutengeneza ajira kwa vijana wetu.
“Mkitupa ridhaa tutaendelea kuwekeza kwa kuongeza tija upatikanaji ruzuku ya mbolea na pembejeo za kilimo. Kama mnavyoona matokeo ya ruzuku na pembejeo za kilimo yameongekana.
Amesema Halmashauri ya Songea imeongeza uzalishaji mazao ya chakula kutoka tani 200,000 hadi tani 455,500.Pia uzalishaji mazao ya kilimo kwa Madaba umepanda kutoka tani 41.7 hadi tani 160,000.
Kwa upande wa Mbinga, uzalishaji kahawa umepanda ambapo pia ruzuku ya miche na pembejeo za kilimo zinatolewa na serikali.
“Uzalishaji kahawa umependa kutoka tani zaidi ya 100 hadi kufikia tani 300,”amesema na kubainisha aliwahi kutembelea shamba la mwekezaji ambalo limeajiri watu 3000 hali inayoonyesha mkoa huo kuwa kinara kwa kilimo.
“Tutajielekeza kujenga viwanda vya kuongeza thamani ili tuongeze ajira nyingi kwa vijana. Niwasisitize ndugu zangu wa Ruvuma mbolea hizi na pembejeo zinazotolewa kwa ruzuku naomba mtumie nyinyi na zisiuzwe.
“Kwa sababu ukiuza unawapa faida wengine wa jirani, mnawapa faida zaidi walime kwao kwa mbolea ya ruzuku, wewe hata ukipata pesa faida zaidi kwa mwenzako,” amesema.
Amewashukuru wananchi wa mkoa huo kwa kuchangia vyema usalama wa chakula ndani ya nchi na mataifa jirani ambako mahindi yanapelekwa kuuzwa.
Aidha amesema Januari mwaka huu Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa nchi 25 za Afrika zinazozalisha kahawa.
Dk. Samia amesema katika mkutano huo liliwekwa lengo la ndani ya miaka 10 ijayo (2025 – 2035) asilimia 50 ya kahawa bora inayozalishwa Afrika iwe inasindikwa kabla ya kuuzwa nje ya Afrika.
“Hilo ndilo lengo la serikali kutekeleza azimio hilo ambapo CCM imeweka ahadi kuweka mitambo ya kukoboa kahawa kabla haijauzwa.
Pia amesema serikali imetekeleza mradi wa ujenzi maghala 28 ya kuhifadhia mazao mkoani Ruvuma ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Songea ina maghala 11, Mabada (tisa) Namtumbo (saba) na ghala moja kwa Manispaa ya Songea.
Mgombea Dk.Samia amesema katika Manispaa ya Songea serikali itakamilisha ujenzi wa soko la kisasa Manzese A na B.”Soko hilo ambalo mmelisubiri kwa muda mrefu sasa linajengwa na hatujawasahau wanangu wamachinga mtakuwa na sehemu katika soko hilo.
“Niseme pia kwamba mkoa huu umebarikiwa kuwa na madini mengi kuanzia dhahabu, shaba, makaa ya mawe, madini ujenzi na vito hadi urani yanapatikana ndani ya mkoa huu,” alisisitiza.
Dk. Samia alieleza kuwa endapo CCM ikipatiwa ridhaa, serikali yake itaanzisha na kuendeleza kongani za viwanda zinazohusiana na madini.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza thamani ya madini kabla ya kuuzwa huku kipaumbele kikiwa katika uchimbaji na wachimbaji wadogo.”Tutakwenda kuboresha wachimbaji wadogo lakini pia tutawaelekeza uchimbaji ambao utatunusuru kwenye vifo.”
Alibainisha kuwa mwaka huu alifika wilayani Namtumbo kuzindua mradi wa madini ya urani pamoja na kuchimba madini hayo azma ya serikali yachakatwe, yasafirishwe kisha uwepo mtambo wa kuzalisha umeme nchini ili umeme wa uhakika upatikane.“Duniani madini hayo yanakubalika kama nishati safi kwa taifa kuyatumia.”