NA JOHN BUKUKU- TUNDURU
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea na kampeni za chama hicho Septemba 22, 2025 katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, ambapo ameahidi kuimarisha zaidi sekta ya elimu kupitia ujenzi wa shule mpya na miundombinu ya kisasa ya sekondari.
Dkt. Samia amebainisha kuwa Tunduru imenufaika kwa kujengewa shule mpya za sekondari nane, mabweni 15, madarasa 253 ya sekondari, shule za msingi nne na madarasa 170, hatua inayolenga kuongeza fursa za elimu na kupunguza changamoto ya msongamano wa wanafunzi.
Mbali na sekta ya elimu, Dkt. Samia aliahidi pia kuimarisha kilimo kwa kujenga skimu mbili mpya za umwagiliaji na kuimarisha zilizopo ili kuwawezesha wakulima kuzalisha mazao kwa ufanisi hata nyakati zisizo za mvua. Aidha, serikali itajenga soko la kisasa na maghala ya kuhifadhia mazao, huku vitalu 221 vikitarajiwa kutoa ajira na kuongeza mapato ya wakazi wa Tunduru.
Akizungumzia sekta ya maji, alisema miradi 31 tayari imetekelezwa na kupelekea upatikanaji wa maji kwa asilimia 85 vijijini na asilimia 78 mjini, huku zaidi ya shilingi bilioni 3.2 zikitengwa kumaliza changamoto kwenye maeneo ya Rahaleo, Masuguru, Mchoteka, Majala, Ligunga na Bugujali.
Katika sekta ya afya, wilaya hiyo imenufaika na ujenzi wa zahanati 18, vituo vya afya vitano na nyumba nne za madaktari, huku serikali ikiwa na mpango wa kujenga zahanati 20 na vituo vya afya vipya. Pia fedha zilizotolewa zimewezesha ukarabati wa hospitali ya wilaya.
Aidha, wananchi wa Tunduru wamenufaika na zaidi ya shilingi bilioni moja kupitia mikopo ya asilimia 10 kwa wafanyabiashara wadogo wadogo.
Kuhusu nishati, Dkt. Samia alisema vijiji vyote tayari vimeunganishwa na umeme na awamu inayofuata itahusisha vitongoji vyote. Pia aliahidi kufufua viwanda vya kubangua korosho vilivyobinafsishwa na kujenga kwa kiwango cha lami barabara zote za Tunduru na Namtumbo.