Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema katika miaka mitano ijayo endapo chama hicho kitapewa ridhaa ya kuongoza nchi, moja ya miradi mikubwa itakayotekelezwa ni ujenzi wa reli ya kisasa itakayounganisha Bandari ya Mtwara na Bandari ya Mbamba Bay mkoani Nyasa.
Amesema kupitia reli hiyo, serikali imelenga kuimarisha usafirishaji wa bidhaa na watu, kukuza biashara ndani na nje ya nchi pamoja na kuifanya mikoa ya kusini kuwa kitovu cha uchumi wa taifa. Aidha, serikali inakusudia kuanzisha kongani kubwa ya viwanda katika ushoroba huo wa kiuchumi, hatua itakayoongeza ajira, kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na kuhamasisha uwekezaji wa kimkakati.
Hayo yameelezwa na Dkt. Samia wakati akizungumza na wananchi wa Mangaka, wilayani Nanyumbu , mkoani Mtwara.