NA JOHN BUKUKU- MTAMA LINDI
Mgombea ubunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye, amesema dhana kubwa inayojitokeza katika uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuweka utu wa Mtanzania mbele ya kila jambo.
Ameyasema hayo Septemba 24, 2025, katika muendelezo wa kampeni za Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Jimbo la Mtama, mkoani Lindi.
Nape Nnauye amesema tangu Rais Samia aingie madarakani mwaka 2021, Serikali imechukua hatua ambazo kimsingi zinalinda hadhi ya mwanadamu na kumfanya Mtanzania ajisikie huru na salama, akibainisha kuwa dhana ya utu kwa Dkt. Samia inajidhihirisha kwa vitendo.
Ameongeza kuwa moja ya mafanikio makubwa ya Dkt. Samia ni kurejesha nafasi ya utu wa Mtanzania katika kila nyanja ya maisha ya kijamii na kisiasa.
Nape pia amesema Dkt. Samia amefungua anga la kisiasa kwa kuruhusu vyama vya siasa kufanya shughuli zao bila hofu, jambo ambalo limejenga imani kwa wananchi kwamba uhuru wa kisiasa upo na unaheshimiwa.
Amebainisha kuwa hatua ya Dkt. Samia kufuta kesi za kisiasa na kuruhusu viongozi wa upinzani waliokuwa wanakabiliwa na kesi kuachiwa huru, ni kielelezo cha kulinda utu na kuheshimu haki za binadamu.
Vilevile, amesema utulivu na mshikamano uliopo sasa ni matokeo ya msimamo wa Dkt. Samia kuongoza kwa hekima, maelewano na kuheshimu utu wa kila raia bila kujali itikadi za kikabila na kidini.
Amehitimisha kwa kueleza kuwa dunia imeshuhudia Tanzania ikifungua ukurasa mpya wa kidemokrasia chini ya uongozi wa Dkt. Samia, ambapo wananchi wanaweza kutoa maoni yao, kufanya mikutano na kushiriki katika mambo ya kijamii bila hofu ya kudhibiwa.