Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said akizindundua Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said akizindundua Mpango wa pili wa utekelezaji Sera ya Hifadhi ya Jamii, Zanzibar, hafla ya uzinduzi imefanyika jana, katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakil, Kikwajuni, kushuto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, na kulia ndugu Khatib Mwadin Khatib Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
…………
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya ustawi na hifadhi ya jamii ili kuhakikisha utimilifu wa afua za hifadhi ya jamii Zanzibar.
Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa SMZ, Mhandisi Zena Ahmed Said, alieleza hayo alipokuwa akizindua Mpango wa Pili wa Utekelezaji wa Sera ya Hifadhi ya Jamii (2025 – 2030) wakati wa Mkutano Mkuu wa Pili wa Mwaka wa Hifadhi ya Jamii uliofanyika ukumbi wa Idriss Abdulwakil, Kikwajuni.
Alisema serikali imeimarisha ustawi wa jamii kwa wananchi bila kujali hali zao, kwa mujibu wa sera ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2014 hivyo kuna haja ya taasisi na wadau kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu.
“Natoa wito kwa wadau wote, taasisi za serikali, washirika wa maendeleo, mashirika ya kiraia na sekta binafsi, kuzidisha mashirikiano katika utekelezaji wa mpango huu kwani hifadhi ya jamii si jukumu la serikali pekee, bali ni jukumu la pamoja kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho”, alisisitiza Mhandisi Zena.
Aidha aliwapongeza wadau hao hasa UNICEF kwa kufanikisha uandaaji wa mpango huo akieleza kuwa nchi imeshuhudia hatua muhimu katika kuimarisha hifadhi ya jamii ili kila Mzanzibari apate heshima na msaada stahiki katika maisha yake.
Aliongeza kuwa utekelezaji wa mpango huu unakwenda sambamba na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 (Vision 2050), Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar (ZADEP) na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) hususani lengo la kutokomeza umasikini na kupunguza pengo la usawa miongoni mwa jamii.
Alifafanua kuwa katika mpango wa kwanza ulifanikisha hatua kadhaa, ikiwemo ya utoaji wa Pensheni Jamii (ZUPS) na kuanzishwa kwa Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) ambapo mpango wa pili unatarajiwa kuziba mapungufu yaliyobainika na kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha, alisisitiza dhamira ya serikali kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi kuhakikisha huduma za ustawi wa jamii zinaboreka zaidi, hasa kwa makundi maalum kama watoto, vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Awali Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Abeida Rashid Abdallah, alieleza kuwa serikali imesema sera ya hifadhi ya jamii imeendelea kuwa dira ya kuhakikisha wananchi hususani makundi yaliyo katika mazingira magumu kama watoto, wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu wanapata huduma za msingi za kijamii kwa heshima na usalama.
Alieleza kuwa sera hiyo inalenga kupunguza umasikini na kukuza usawa kwa kuchangia usalama wa kipato, kutoa ulinzi dhidi ya misukosuko ya maisha na kupanua huduma za kijamii kwa wananchi wote.
“Kukamilika kwa mpango wa kwanza wa utekelezaji wa miaka mitano uliofikia mwaka 2022 na kumeleta mafanikio makubwa, ikiwemo ya misaada ya fedha kwa kaya maskini kupitia TASAF (Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania), huduma za ustawi wa jamii, kuimarika kwa hifadhi ya mtoto Zanzibar na kuanzishwa kwa mpango wa pensheni ya jamii (ZUPS)”, alieleza Abeida.
Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya serikali na wadau umesaidia kuimarisha uratibu wa huduma hizo, hivyo hatua hiyo inatarajiwa kuongeza kasi ya maendeleo ya kijamii katika awamu inayofuata ya utekelezaji wa sera.
Akizungumzia katika uzinduzi huo Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) ofisi ya Zanzibar, Laxmi Bhawani, alisema mpango huo ni wa kipekee kutokana na kuzingatia usajili wa jamii kitaifa na kutumia mifumo ya malipo ya kielektroniki, hatua ambayo inayoimarisha utoaji huduma kwa walengwa.
Aliongeza kuwa mpango unaweka mpango thabiti wa ufadhili ili kuhakikisha uendelevu na kutabirika kwa afua za ulinzi wa kijamii na unasisitiza uratibu wa sekta mbali mbali, mawasiliano ya kimkakati na ulinzi wa kisheria, kuweka vigezo muhimu katika kutoa huduma jumuishi na kuimarisha matokeo ya kijamii.
“Nguzo ya hifadhi ya jamii ya Zanzibar ipo katika mshikamano wetu wa pamoja hivyo UNICEF itaendelea kushirikiana na serikali pamoja na wadau wote ili kupanua wigo, kuimarisha ubora na kuhakikisha ulinzi wa jamii unawafikia watoto, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu”, alieleza Laxmi.
Aidha aliipongeza serikali kwa hatua kubwa ilizozifikia, huku ikisisitiza mshikamano wa pamoja katika kujenga Zanzibar jumuishi, imara na yenye usawa ambapo kila mtoto ana nafasi ya kustawi na kufikia uwezo wake kamili.