Na Meleka Kulwa -Dodoma
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amewataka waandishi wa habari kuhakikisha wanazingatia maadili na uhalisia katika kuripoti habari za uchaguzi ili kusaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi.
Waziri Mavunde ametoa kauli hiyo Septemba 27, 2025 kwakati akifungua Mafunzo ya waandishi wa Habari kuhusu masuala ya Uchaguzi na Usalama kwa waandishi wa habari mkoani Dodoma yaliyoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dodoma (DPC), Waziri Mavunde amesema kuwa tasnia ya habari ni nguzo muhimu hasa kuelekea kipindi cha uchaguzi.
“Waandishi wa habari ni watu muhimu sana katika jamii. Taarifa isiyo sahihi inaweza kusababisha hata uvunjifu wa amani. Niwaombe tuendelee kuzingatia maadili, tusimame katika taaluma yetu na tufanye kazi kwa usawa bila upendeleo,” amesema.
Aidha, amewakumbusha waandishi wa habari kuwa jamii inawategemea kupata taarifa sahihi zinazozingatia ukweli na maadili ili wananchi waweze kufanya maamuzi ya busara katika kuwachagua viongozi wao.
“Wakati mwingine mtu anampenda mgombea na kuandika amepokewa na mafuriko ya watu, lakini picha zikionekana hazizidi watu hamsini. Hii haijengi heshima. Twendeni tuka ripoti mambo yote katika uhalisia wake na tuwasaidie wananchi kufanya maamuzi sahihi,” amesema Waziri Mavunde
Aidha, Waziri Mavunde amewahimiza waandishi wa habari kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha wananchi kutumia haki yao ya kikatiba kushiriki uchaguzi.
“Watanzania lazima washiriki kwenye uchaguzi, nyie wanahabari wasaidieni kujua umuhimu wa uchaguzi na kushiriki kupiga kura kwa kuchagua Viongozi wao kwa miaka mingine mitano.
Waziri Mavunde ameongeza kuwa ni wajibu wa waandishi wa habari wa Mkoa wa Dodoma kuwasaidia wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu changamoto wanazokabiliana nazo na ahadi za wagombea katika kuzitatua.
“Niwaombe sana tuisaidie jamii ya Dodoma kupata taarifa za kweli ili kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi. Sio Dodoma pekee, bali pia Watanzania kwa ujumla,” amesema Waziri Mavunde.
Awali akizungumza, Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Dodoma ( DPC,) Katare Mbashiru, amesema kuwa kongamano hilo limekuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu bora za kuripoti habari za uchaguzi kwa weledi na kuzingatia misingi ya taaluma ya uandishi, amesema
”mafunzo hayo yataleta tija kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Dodoma katika kuhakikisha wanabaki kuwa waandishi wa kuaminika na walinzi wa demokrasia”.
Aidha, Katare Mbashiru, amebainisha kuwa kupitia mafunzo hayo, waandishi wa habari wataongeza uelewa kuhusu maadili, sheria na kanuni za uchaguzi, pamoja na mbinu za kutumia teknolojia katika upashanaji wa habari, jambo litakaloongeza mchango wao katika kudumisha demokrasia na kuimarisha mshikamano miongoni mwao.