Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa 2025 Ismail Ali Ussi wakati akizungumza na wakazi wa Kijiji Cha Kanondo manispaa ya Sumbawanga.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika soko la mazao Kanondo wakishuhudia uwekaji wa jiwe la msingi.
Na Neema Mtuka Sumbawanga
Rukwa:Soko jipya la kisasa la mazao limezinduliwa likiwa na miundombinu ya kisasa na uwekezaji wenye thamani ya sh bill 7.3 hatua inayotarajiwa kuongeza thamani ya mazao ya wakulima, kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi.
Uzinduzi huo umefanyika katika kijiji cha Kanondo kata ya Ntendo Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.
Akizungumza leo Septemba 29, 2025 wakati wa uzinduzi huo, afisa wa mradi huo Mhandisi John Myovela ameeleza kuwa soko hilo limejengwa kwa ubora wa kisasa likiwa na maghala, sehemu za kuhifadhia mazao na huduma muhimu kwa wafanyabiashara, na litawezesha wakulima kupata bei bora za mazao yao sambamba na kuchangia pato la taifa.
“Kukamilika kwa ujenzi wa soko hilo la kisasa kutachochea uwekezaji na wakulima watapata fursa ya kuuza mazao yao katika soko hili” amesema Myovela
Kwa upande wake, kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 Ismail Ali Ussi amesifu mradi huo, akibainisha kuwa wananchi watanufaika kupitia fursa mbalimbali zikiwemo ajira, biashara ndogondogo na uongezaji thamani wa mazao, jambo litakalosaidia kupunguza umasikini.
Nao wananchi walioshuhudia uwekwaji wa jiwe la msingi wa soko hilo akiwemo Agneta Nzelani ameeleza furaha yake na kuishukuru serikali kwa utekelezaji wa mradi huo, akisema kuwa soko limekuja kama suluhisho la changamoto ya muda mrefu ya masoko na litafungua fursa mpya za kimaendeleo katika jamii.
“Soko hili ni fursa kwa wakazi wa manispaa ya Sumbawanga kwa kuwa utawavutia wawekezaji na kutuondolea changamoto ya kuuza mazao yetu kwa walanguzi.amesema Nzelani.
Soko hilo likikamilika litawanufaisha wakazi wa mkoa wa Rukwa kwa kuwa soko hilo litafungua biashara na ajira kwa vijana na kuufungua mkoa wa Rukwa.
Mwenge wa Uhuru unaendelea na mbio zake mkoani Rukwa, ambapo unatarajiwa kukimbizwa katika miradi mingine ya kijamii na kiuchumi katika siku chache zijazo.