Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Katibu Mkuu wizara ya maliasili na utalii Nchini Dkt.Hassan Abbas amekabidhi vifaa mbalimbali kwaajili ya kufukuzia tembo kwenye makazi ya wananchi waishio kandokando ya hifadhi ya Taifa mkomazi.
Akizungumza katika moja ya kituo cha askari wa uhifadhi ndani ya hifadhi ya Taifa mkomazi kilichopo eneo la Goha wilayani Korogwe Mkoani Tanga Dkt.Abbas amesema serikali inaendelea kuchukua hatua zaidi za kupata muarobaini wa changamoto ya tembo kwenye makazi na mashamba ya wananchi waishio kandokando ya hifadhi kote Nchini.
Amesema kutokana na tembo kuendelea kuwa tishio kwa wananchi na kufanya uharibufu mkubwa wa mali za wananchi serikali imeendelea kubuni mbinu mbalimbali za kukabiliana na wanyama hao ili kuondoa adha kwa wananchi huku akisema kuongezeka kwa mwingiliano wa tembo na wananchi kumesababishwa na uwepo wa vijiji vingi vilivyoanzishwa kandokando ya hifadhi.
“Leo tumekabidhi vifaa hivi kwaajili ya kuwasaidia askari kufanya doria ya tembo kwenye makazi ya wananchi wetu na pindi wanapoonekana basi vifaa hivi hutumika kuwarudisha hifadhini lakini pia uwepo wa ongezeko kubwa la tembo kwenye makazi ya wananchi hii husababishwa na wanyama hawa wanaishi kwa kumbukumbu kubwa mno eneo alilopita tembo zamani hata ipite miaka zaidi ya 40 arudia pale tena hilo la kwanza lakini pia wapo wanyama wengine huingia Kutoka hifadhi ya nchi jirani na wataalam wetu wanafanya tafiti ili kujua wanyama ambao asili yake ni mkomazi na tutafanya mpango wa kuwahamishia hifadhi nyingine “”Alisema Dkt.Abbas”.
Miongoni mwa vifaa vilivyokabidhiwa kwa Mkuu wa hifadhi ya Mkomazi ni pamoja na ndege nyuki,mabomu baridi pamoja na pikipiki mbili za doria kwa askari wa uhifadhi.