NA DENIS MLOWE , IRINGA
MGOMBEA anayepewa nafasi kubwa kuibuka na ubunge jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi, Fadhili Ngajilo amesema atatumia uwingi wa vyuo vikuu mkoani hapa kuibadilisha Iringa kuchochea maendeleo.
Akizungumza wakati wa kampeni za jimbo hilo katika kata ya Gangilonga uliofanyika katika viwanja vya Sabasaba Ngajilo alisema kuwa kupitia vyuo vikuu tutashirikiana navyo vyema kwani ni chachu ya maendeleo kutokana na kuzalisha wasomi na wabunifu.
Alisema kuwa endapo watamchagua kuwa Mbunge atahakikisha anakaa na vyuo mbalimbali vilivyopo hapa ili kuzungumza namna ya kushiriki katika kuubadilisha Iringa kwenye sekta mbalimbali kutokana na uwezo katika ubunifu na kuzalisha wasomi.
Alisema kuwa uwepo wa vyuo mkoani hapa ni ishara tosha ya mkoa kuwa na rasimali watu ambao wakitumika vyema katika kubuni mikakati ya maendeleo Iringa itabadilika kwa haraka.
“Nitahakikisha nashirikiana vyema na vyuo vikuu kwa kuwa nami nimepita chuo kwa kusoma na kufundisha hivyo tutakaa nao chini katika kupanga mikakati ambayo itawezesha Iringa kuwa na maendeleo kwani kule wanazalisha wabunifu ambao wataleta tija katika maendeleo ya jimbo la Iringa” Alisema
Aidha Ngajilo aliongeza kuwa kata ya Gangilonga ina uwingi wa benki hivyo kupitia hilo atahakikisha anatumia vyema uwingi huo kuzungumza na benki hizo katika mikopo rafiki kwa makundi mbalimbali hasa wajasiriamali.
Akizungumzia ahadi za mgombea udiwani wa kata ya Gangilonga Liikotiko Kenyata, Ngajilo alisema kuwa atahakikisha wanashirikiana kutatua changamoto zote zinazoikabili kata hiyo.
Kwa upande wake mgombea udiwani wa kata ya Gangilonga, Likotiko Kenyata alisema kuwa endapo atachaguliwa atakamilisha miradi ambayo alikwisha ianzisha ikiwemo Milioni 246 kujenga madarasa ya awali manne, jengo la utawala na matundu ya vyoo katika shule ya Lugalo.
Alisema kuwa atahakikisha anawezesha wananchi kiuchumi , mitaji, na mikopo nafuu na kurasimisha makazi kwenye mtaa wa Lugalo B.