
Lissu ameiwasilisha hoja tatu mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru akisaidiana na Jaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam akidai kwamba anataka ufafanuzi kwanza ndiyo kesi hiyo iweze kuendelee na hatua ya usikilizwaji.
“Nipo tayari kuendelea kusikilizwa kwa kesi lakini kabla hatujaanza nina mambo matatu naomba Mahakama inipatie maelezo, Septemba 30, 2025 Naibu Msajili Livin Lyakinana aliniandikia
Lissu amesema alipokea wito wa kesi (summons) kutoka kwa Naibu msajili ukionesha kuwa shauri hilo lingesikilizwa kuanzia Oktoba 6 hadi Oktoba 24, kisha likapumzika kwa siku kumi na kuendelea tena kuanzia Novemba 3 hadi 11.
Hata hivyo, alisema kwa mshangao mkubwa, alipokea (cause list) iliyoonesha kwamba hukumu ya kesi hiyo itatolewa Novemba 12, 2025.
“Kesi hii haijasikilizwa shahidi hata mmoja, lakini tayari imepangwa tarehe ya hukumu. Kama hukumu ipo tayari basi itolewe. Nataka kujua, ni nani anapanga ratiba ya mahakama hadi kufikia tarehe ya hukumu wakati kesi yenyewe haijaanza kusikilizwa?” alihoji Lissu mbele ya majaji wa kesi hiyo.
Katika hoja yake ya kwanza, Lissu alisema alielekezwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, kwa barua ya tarehe Septemba 30, kwamba aandike majina ya watu 100 ambao angependa wahudhurie kesi yake — wakiwemo mawakili, viongozi wa chama, wanachama na ndugu zake
Alisema alipokea barua hiyo akiwa Gereza la Ukonga kupitia mkuu wa gereza Oktoba 2, na akatakiwa kuwasilisha majina hayo kabla ya saa 12 jioni Oktoba 3.
“Nilitekeleza agizo hilo, niliandika majina ya watu hao. Lakini leo nimeona mwenyewe baadhi yao wakizuiliwa na polisi kwenye lango la mahakama,” alisema.
“Mmoja wao ni Dkt. Stephanie kutoka Ujerumani ambaye nimemuona akiwa nje amezuiwa kuingia. Mwingine ni Keith kutoka Washington DC, ambaye kama ningejua angekuja, ningemweka kwenye orodha,” alisema Lissu.
“Naomba kujua hii ni Mahakama Kuu ya Tanzania au mahakama ya polisi. Nani anaamua nani aingie na nani asiingie? Kama polisi ndio wanaamua, basi tujue. Maana kama majina niliyotoa hayaheshimiwi, maana ya barua ya Msajili ni nini?”
Pia Lissu alieleza kuwa Oktoba Mosi, 20225 alipokea barua nyingine kutoka kwa Naibu Msajili iliyomtaka kushiriki kikao cha “pre-session meeting” kupitia mtandao siku hiyo hiyo ya Ijumaa Oktoba 3 saa nane mchana, muda wa saa mbili tu baada ya kupokea barua.
Alisema hali hiyo ilimshangaza kwa kuwa akiwa gerezani hana maandalizi wala mawasiliano ya haraka.
“Nilimwambia ninahitaji taarifa sahihi mapema (‘proper notice’). Hata kama niko gerezani, notice ya masaa mawili haiwezekani. Naomba maelekezo, hiyo pre-session ni nini kisheria? Kwa uelewa wangu, baada kusomwa kwa maelezo ya awali (preliminary hearing) kumalizika, kesi inatakiwa kuanza kusikilizwa siyo presession tena,” alisema.
Baada ya Lissu kumaliza kutoa hoja hizo, Jaji Ndunguru alikuja na uamuzi kwamba utaratibu anaolalamikia mshtakiwa ni wa kawaida kwa mujibu wa sheria.
Kuhusu hoja ya kwamba baadhi ya watu wake waliokuja kusikiliza kesi alisema Septemba 16,2025, Mahakama ilitoa maelekezo namna watu watakavyoweza kuhudhuria kwenye kesi bila kuharibu taratibu zingine za Mahakama na kwamba utaratibu uliotolewa uzingatiwe.