Na Ashrack Miraji
WATU waliojichukulia sheria mkononi wamemuuwa aliyekuwa Mgombea wa Ubunge Jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro kupitia Chama Cha Wananchi CUF, Daud Ntuyehabi.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, SACP Simon Maigwa alisema kuwa, tukio hilo lilitokea Oktoba 7 mwaka huu majira ya 1:30 usiku katika Kijiji cha Kilingi Sanya juu wilayani Siha.
Alisema kuwa, tukio hilo la kujichukulia sheria mkononi limetokea baada ya Daudi Ntuyehabi kumchoma kwa kisu tumboni Abdul Mohamed mkazi wa Kilingi kata ya Sanya juu na kusababisha utumbo kutoka nje.
Kamanda Maigwa aliendelea kubainisha kuwa, inadaiwa sababu zilizopelekea Abdul kuchomwa kwa kisu ambaye bado anaendelea na matibabu hospitali ni kitendo chake cha kwenda kuamulia ugomvi uliozuka kati ya Daudi Ntuyehabi na Hamadi Mohamed wakati wanakunywa pombe kwenye grocery kutokana na kudaiana fedha.