Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Comoro, Mheshimiwa Saidi Othman Yakubu, ametembelea Hospitali ya Bambao katika Kisiwa cha Anjouan kukagua maendeleo ya Kambi Tiba inayoendelea hospitalini hapo, inayotekelezwa na madaktari bingwa kutoka Tanzania kwa ushirikiano na wenzao wa Comoro.
Katika ziara hiyo, Balozi Yakubu alipokelewa na viongozi wa afya wa Anjouan na kutembelea wodi mbalimbali, ambako alizungumza na wagonjwa na wahudumu wa afya walioko katika huduma.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mheshimiwa Yakubu alisema kuwa Tanzania na Comoro zinaendeleza ushirikiano wa kihistoria unaolenga kuboresha ustawi wa wananchi, hususan katika sekta ya afya.
“Tunajivunia kuona madaktari wetu wa Tanzania wakishirikiana na wenzao wa Comoro kutoa huduma bora kwa wananchi wa Anjouan. Huu ni uthibitisho wa urafiki wa kweli na dhamira ya pamoja ya kujenga afya ya watu wetu,” alisema Balozi Yakubu.
Kambi Tiba hiyo inahusisha huduma za upasuaji, uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza, huduma za afya ya mama na mtoto, pamoja na elimu kwa jamii kuhusu kinga na matibabu.
Kwa upande wake, uongozi wa Hospitali ya Bambao ulitoa shukrani kwa Serikali ya Tanzania na Balozi Yakubu kwa mchango wao katika kuboresha huduma za afya nchini Comoro.
Kambi Tiba hii ni sehemu ya utekelezaji wa ushirikiano wa sekta ya afya kati ya Tanzania na Comoro, chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mhe. Kanali Azali Assoumani.