…………..
NA DENIS MLOWE, IRINGA
BENKI Azania tawi la Iringa imeadhimisha wiki ya huduma kwa mteja lengo kuu likiwa ni kuwashukuru wateja wake kwa kuwa nao bega kwa bega katika ukuaji wa benki hiyo mkoani hapa.
Maadhimisho hayo yaliyofika kelele leo na mgeni rasmi alikuwa mkuu wa mkoa wa Iringa Kheri James aliyeambatana na wateja mbalimbali wa benki hiyo.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa , Kheri James aliwataka wajasiriamalii kuepuka wakopeshaji vishoka maarufu kama kausha damu na kutumia benki hiyo kwa kutokana na riba ndogo na uaminifu kujiletea maendeleo.
Alisema kuwa wananchi na wajasiriamali mkoani hapa watumie huduma za kibenki zilizo kwa wingi kuepukana na unyonyaji unaofanywa na watu wasio na nia njema kwao mwisho wa siku wanalizwa.
“Najua fika kwamba kusogezewa karibu huduma za kifedha ikiwemo uwingi wa benki mkoani hapa ni fursa kubwa kiuchumi hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kutumia ipasavyo uwepo wa huduma hizi kwa wananchi ” Alisema
Aliongeza kuwa kutumia vema uwepo wa benki kama hii ya Azania kwa kutunza akiba zenu na pia kukopa ili kuwekeza na kukuza biashara zenu itasaidia kukua kwa uchumi wa kila mmoja na taifa kwa ujumla.
Hata hivyo Kheri James alitoa rai kwa benki hiyo kuendelea kubuni mipango mbalimbali ya utoaji wa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kutumia benki sambamba na kubuni huduma zinazowagusa wananchi wa wenye hali ya kawaida kiuchumi ili waweze kutumia vema fursa na huduma zinazotolewa na benki hiyo. Hususani katika mikopo.
Alisema kuwa katika kutoa elimu hiyo angalieni fursa ambazo zinapatikana kwa wingi mkoani hapa kama vile ujenzi wa hotel kubwa ambazo zinaweza chukua watu hata 1000 kwa siku, kumbi ambazo zinaweza beba watu 2000 na sehemu nyingi ukigusa zinafursa hivyo jukumu la benki kutoa mikopo kwa kuangalia fursa kama hizo.
Kwa upande wake Meneja wa Benki hiyo tawi la Iringa, Gaile Lungwa alisema kuwa hiyo inamilikiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwemo NSSF PSSSF,NHIF wamejipanga kutoa huduma bora kwa wateja na zenye riba nafuu hivyo wana wajibu mkubwa wa kusaidiana na serikali katika kuendeleza umma wa watanzania.
Alisema kuwa benki ya Azania imeelekeza nguvu zake katika kuhakikisha kila mteja anapata huduma bora kulingana na mahitaji yake na wanahudumia aina zote za wateja wakiwemo wakulima na wafugaji.
Alisema kuwa mwaka huu benki ya Azania wamekuja na kauli mbiu inayosema Ni Mission Possible hivyo wamefanikiwa kuwafikia wateja katika wilaya zote za mkoa wa Iringa na kama Azania wamejikita katika huduma za akaunti mbalimbali, mikopo ya aina mbalimbali hususani ya kilimo na ufugaji
Vile vile alisema kuwa wana mikopo ya wakina mama yenye riba nafuu ya asilimia moja kwa mwezi lakiini pia wana mikopo ya wastaafu yenye riba ndogo sana kwa kuamini kwamba ukistaafu bado una fursa ya kuendelea kufanikiwa.
Aidha aliongeza kuwa tangu kufunguliwa kwake Aprili 4 mwaka huu Azania tawi la Iringa wamefanikiwa kutoa mikopo ya zaidi ya bilioni 3 kwa kipindi cha miezi 6 na wanufaikaji wengi wamekuwa wakinamama,wafanyakazi ,wakulima wafugaji,wastaafu, vijana na makundi mengine mkoani hapa.