Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dennis Gondwe akifafanua jambo kuhusu Wiki ya Huduma kwa Mteja ofisini kwake
Na. Leah Mabalwe, DODOMA
Halmashauri ya Jiji la Dodoma inatumia maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja kutathmini mfumo wa utoaji huduma kwa wananchi na kuhamasisha mawasiliano bora ili kuwaweka wananchi karibu zaidi na halmashauri yao.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dennis Gondwe, alipokuwa akijibu swali la jinsi halmashauri inavyotumia maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja ofisini kwake.
Gondwe alisema kuwa Wiki ya Huduma kwa Mteja ni wiki inayoikumbusha halmashauri kuwa ipo kwa ajili ya utoaji huduma kwa wananchi. “Msingi wa uwepo wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni utoaji wa huduma bora na za viwango kwa wananchi. Ni kipindi ambacho tunatafakari hali ya huduma tunayotoa kwa wananchi, ni kipindi ambacho tunatafakari kule tunapolenga kufika katika viwango vya utoaji wa huduma.
Menejimenti ya halmashauri inalenga kufika sehemu ambapo malalamiko ya huduma zinazotolewa kwa wananchi inakuwa ni historia.
Tunataka kufika sehemu ambapo mwananchi hakumbuki mara ya mwisho ilikuwa lini kupata huduma chini ya kiwango, mara ya mwisho lini kupanga foleni kusubiri huduma” alisema Gondwe.
Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeanzisha mfumo wa utoaji huduma kupitia kanda. “Jumla ya kanda saba za utoaji huduma zimeundwa kwa lengo la kuwasogezea huduma wananchi karibu na maeneo waliyopo.
Halmashauri imewafuata wananchi walipo, hivyo, tunaongelea huduma karibu na wananchi, tunaongelea huduma ndani ya muda mfupi, tunaongelea huduma bila kutumia gharama na muda kuifuata, hii ndiyo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Tunatumia wiki hii ya huduma kwa mteja, kuboresha zaidi mawasiliano yetu na wananchi ambao tunawahudumia, kwa kuwasikiliza, kushauriana nao na kupata mrejesho wa huduma tunazotoa ili tuendelee kuwa bora zaidi.
Maadhimisho haya yanafanyika hapa ofisi kuu na katika ofisi zetu zote za kanda” alisisitiza Gondwe.
Katika hatua nyingine, mkazi wa Kata ya Iyumbu, Lucas Moses alieleza kuwa mfumo wa utoaji huduma kupitia kanda umeboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, kwasababu wanahudumiwa karibu na makazi yao jambo lililopunguza muda na gharama. “Kupitia mfumo wa kanda, tunapata huduma karibu na haraka zaidi. Tunashauri maboresho zaidi kwenye miundombinu” alisema Moses.
Kwa upande wake, mfanyabiashara Edmund Mngassa aliyeenda kupata huduma katika Ofisi ya Kanda Namba Moja, alipongeza huduma bora aliyopata katika Kanda Namba Moja, akisema kuwa zimekuwa chachu ya mabadiliko katika safari yake ya kibiashara.
“Sikuwahi kufikiria kuwa ningeweza kupata huduma nyingi kiasi hiki sehemu moja na ndani ya muda mfupi. Zaidi ya yote nimepokelewa vizuri, lakini pia kuna baadhi ya vitu ambavyo nilikuwa sina uelewa navyo maafisa wameweza kunielewesha.
Hivyo, niwasisitize wafanyabiashara wenzangu tusikae nyuma, tuje kukata leseni za biashara na huduma zingine ili tuweze kufanya biashara kwa uhalali’’ alisema Mngassa.