Na John Bukuku, Dar es Salaam
Wadau wa maendeleo nchini wamekubaliana kuwa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) una nafasi muhimu katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika kuchochea ukuaji wa uchumi jumuishi na kuboresha ustawi wa wananchi.
Hayo yamebainishwa katika majumuisho ya Kongamano la Nafasi ya PPP katika Kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, lililowakutanisha wataalam, watunga sera, wawakilishi wa sekta binafsi na taasisi za elimu kujadili mchango wa ubia katika utekelezaji wa dira hiyo ya muda mrefu ya taifa.
Katika majadiliano hayo, imeelezwa kuwa ubia wa sekta ya umma na binafsi siyo ubinafsishaji au uuzaji wa mali za serikali, bali ni ushirikiano wa kimkakati unaolenga kugawana majukumu na rasilimali kwa lengo la kufanikisha maendeleo endelevu.
Wanakongamano wamesisitiza kuwa ubia huo unaipunguzia serikali mzigo wa kifedha katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, kwani sekta binafsi inaweza kushiriki kufadhili na kusimamia miradi hiyo kwa ufanisi zaidi.
Aidha, wamesema maeneo mengi ya ndani ya halmashauri yanaweza kunufaika na ushirikiano huo, ikiwemo ujenzi wa masoko, maegesho na miundombinu ya kijamii, ambayo yangeweza kufanyika kwa ubia badala ya serikali kutumia fedha zake pekee.
Akizungumzia sekta ya elimu, imesisitizwa kuwa ubia ni muhimu katika kufanikisha malengo ya Dira 2050, kwani elimu ndio nguzo kuu ya maendeleo ya taifa. Wamesema mabadiliko ya mtaala kutoka mfumo wa maarifa kwenda mfumo wa umahiri yanahitaji uwekezaji mkubwa katika kuwajengea uwezo walimu, sambamba na kuhimiza maadili na thamani miongoni mwa wanafunzi.
Pia, wanakongamano wamependekeza kuboreshwa kwa mkakati wa mawasiliano kuhusu miradi ya PPP, ili kuongeza uelewa wa wananchi na kuhakikisha ushirikishwaji wa makundi yote katika jamii.
Vilevile, imeelezwa kuwa utekelezaji wa Dira 2050 unahitaji kuzingatia utawala bora, umoja wa kitaifa, uwazi, ushirikiano na mapambano dhidi ya rushwa, huku serikali za mitaa zikihusishwa kikamilifu katika utekelezaji wake.
Kwa upande wa uchumi, washiriki wamesisitiza kuwa uchumi jumuishi ni ule unaowapa fursa Watanzania wengi kushiriki moja kwa moja katika shughuli za uzalishaji, hususan kupitia kuboresha tija katika sekta ya kilimo ambayo inawaajiri Watanzania wengi.
Wamesema ili kufanikisha hayo, miundombinu ya umwagiliaji lazima iongezwe na teknolojia za kisasa ziongezwe katika kilimo, sambamba na ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji wa thamani ya mazao.
Kongamano hilo limehitimishwa kwa wito wa pamoja wa kuimarisha ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, ili kuhakikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inatekelezwa kwa ufanisi na kuleta maendeleo endelevu kwa Watanzania wote.