Mgombea ubunge wa Jimbo la Peramiho na Waziri wa Afya Jenista Mhagama, amewahakikishia wananchi wa kata ya Mbinga-Mhalule, kuwa serikali ya Chama Cha Mapinduzi CCM imejipanga kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wote, ikiwa ni pamoja na kugharamia matibabu ya magonjwa kama figo, saratani, kisukari, magonjwa ya moyo n.k.
Akizungumza katika mikutano ya kampeni, kwenye Vijiji vya Lipokela, Mbinga_Mhalule na Nakahegwa, Jenista alisema kuwa ilani mpya ya CCM imeweka msukumo mkubwa katika kuhakikisha wananchi wote wanapata bima ya afya kwa wote, hatua itakayowawezesha hasa wananchi wa kipato cha chini kupata matibabu bila kikwazo cha gharama kubwa.
Alibainisha kuwa mgombea urais wa CCM Samia Suluhu Hassan, ameahidi ndani ya siku 100 za mwanzo wa uongozi wake, wananchi wote wanaosumbuliwa na magonjwa hayo watatibiwa bure kwa ufadhili wa serikali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za afya kwa Watanzania.
Jenista aliwataka wananchi kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura tarehe 29 Oktoba na kuwachagua wagombea wa CCM ili kuhakikisha sera hizo bora zinaendelea kutekelezwa kwa vitendo katika maeneo yote ya nchi.
Aliwahimiza wakazi wa Peramiho kuwapa kura za heshima wagombea wa CCM, akisisitiza kuwa ushindi wa Samia ni ushindi wa wananchi wa Ruvuma pia, kutokana na ukweli kuwa mgombea mwenza wa urais kupitia CCM, Balozi Emmanuel Nchimbi, anatoka katika mkoa huo.
Kwa ujumla, Jenista alisisitiza kuwa CCM ndio chama chenye uwezo wa kweli kuleta maendeleo ya watu, hasa katika nyanja muhimu kama afya, elimu na miundombinu, hivyo wananchi wasikose nafasi ya kuchagua maendeleo.