Na Silivia Amandius
Kagera.
Vijana nchini wamehimizwa kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, ili kuonesha uzalendo na umoja wa kweli wa Watanzania.
Akizungumza katika mkutano wa hamasa kwa vijana, Mwenyekiti wa Kampeni ya Mama Asemewe na Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), Geofrey Kiliba, alisema vijana wana nafasi ya kipekee katika kujenga taifa lenye demokrasia na maendeleo endelevu kupitia ushiriki wa amani kwenye uchaguzi.
Kiliba alisisitiza kuwa nguvu, ubunifu na ushawishi wa vijana ni silaha muhimu katika kuhamasisha jamii kushiriki kupiga kura kwa utulivu, huku akihimiza kundi hilo kutumia fursa hiyo kuchagua viongozi wenye maono na uzalendo wa kweli.
“Vijana ndiyo injini ya taifa letu. Tukishiriki kwa amani na umoja, tutakuwa sehemu ya historia ya kuleta mabadiliko chanya kwa nchi yetu,” alisema.
Baadhi ya vijana walioshiriki mkutano huo waliipongeza serikali na vyombo vya ulinzi kwa kuendelea kuhakikisha maandalizi ya uchaguzi yanafanyika kwa usalama, huku wakiahidi kuwa mabalozi wa amani, upendo na mshikamano katika jamii zao.
Walisema wataendelea kutoa elimu kwa wenzao kuhusu umuhimu wa kuepuka maneno ya uchochezi na badala yake kushiriki katika siasa za hoja, wakisisitiza kuwa uchaguzi wa 2025 unapaswa kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika kwa misingi ya amani, haki na umoja wa kitaifa.