Mganga kiongozi wa Zahanati ya Lugali kata ya Mkumbi Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma Theodora Lusendamila, akimuhudumia mgonjwa aiyefik katika zahanati hiyo. |
Katibu wa afya wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma George Mhina kulia,akizungumza na baadhi ya wagonjwa waliofika kupata huduma za matibabu katika zahanati ya Lugali.
………
Na Mwandishi Wetu, Mbinga
WANANCHI wa Kijiji cha Lugali kata ya Mkumbi Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma,wamefurahishwa na hatua ya Serikali kukamilisha ujenzi wa Zahanati yao na hivyo kumaliza mateso ya muda ya kutembea umbali mrefu ili kufuata huduma za matibabu.
Wamesema,kukamilika kwa zahanati yao kumewapa fursa kwao kufanya shughuli za kujiletea maendeleo ikiwemo kilimo,tofauti na miaka ya nyuma ambapo watumia muda wao kwenda kufuata matibabu makao makuu ya kata Mkumbi au Hospitali ya Wilaya Mbinga mjini.
Lucy Ndunguru alisema,kwa sasa zahanati hiyo imewaondolea kero ya kupata huduma za afya mbali na makazi yao hasa akina mama na watoto wadogo ambao walishindwa Kwenda vijiji vingine kufuata huduma hizo.
Alisema,tangu zahanati hiyo ifunguliwe wanapata huduma karibu na kuishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa fedha na Halmashauri ya Wilaya Mbinga kwa kusimamizi vyema ujenzi wa mradi huo.
Fidea Kapinga alisema,kabla ya zahanati hiyo haijafunguliwa walikuwa kwenye mateso makubwa kwa kutembea zaidi ya kilometa 3 kwenda Mkumbi lakini sasa huduma zote muhimu wanazipata katika Kijiji chao.
“Sisi mama wajawazito na watoto ndiyo tulioteseka sana kwa kutembea umbali mrefu kwenda Mkumbi au Hospitali ya Wilaya Mbinga mjini kwa ajili ya kufuata matibabu,tunaishukuru sana Halmashauri ya Wilaya kwa kusimamizi vyema zahanati yetu”alisema Kapinga.
Kwa upande wake Mganga wa Zahanati hiyo Theodora Lusendamila,amewapngeza wananchi wa Kijiji hicho kujitolea nguvu zao zilizofanikisha ujenzi wa zahanati ambayo imekuwa msaada mkubwa kwao kwa kupata huduma za matibabu karibu na makazi yao.
Alisema,mwanzoni wananchi wa Lugali walikwenda vijiji vingine kufuata huduma za matibabu lakini kukamilikwa zahanati hiyo kumewasaidia kumaliza changamoto iliyokuwepo na sasa wanapata huduma bora hivyo kutoa fursa kufanya kazi za kujiletea maendeleo.
“Kabla ya kujengwa kwa zahanati hii wananchi hususani mama wajawazito walikuwa kwenye mateso makubwa kwani wapo waliojifungulia njiani wakati wanakwenda kwenye vituo vya kutolea huduma hasa ikizingatia usafiri ulikuwa shida na barabara ni mbovu,kwa hiyo zahanati hii imemaliza sana mateso kwa wananchi wa Kijiji hiki”alisema Lusendamila.
Lusendamila,ameishukuru Halmashauri ya Wilaya Mbinga kwa kuona umuhimu wa kumalizia ujenzi wa zahanati hiyo ambayo iliyoanza kujengwa na wananchi,na kupeleka dawa zote muhimu pamoja na vifaa tiba vinavyowezesha wananchi kupata huduma bora za matibabu.
Lusendamila ametaja magonjwa makubwa yanayowakabili wananchi wanaofika kutibiwa kwenye zahanati hiyo ni ngozi hasa kwa watoto wadogo,nimonia,na malaria ambapo amewatoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanakwenda kupata huduma katika zahanati hiyo badala ya kutumia dawa za asili ambazo hazina uhakika wa kutibu maradhi.
Katibu wa afya wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga George Mhina mehaidi kuwa,Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya itaendelea kuboresha huduma za matibabu ka kuleta dawa na vifaa tiba ili wananchi waweze kupata huduma bora na kwa wakati.
Alisema,tangu zahanati hiyo ilipofungiwa mwezi Februari mwaka huu wananchi wa Lugali na vijiji vingine vya jirani wanafurahia huduma zinazotolewa na kuwataka wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali yao ya kuboresha huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo afya.