Na Mwandishi Wetu, WMTH, Songwe.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha watanzania wote, hususan wanaoishi vijijini na maeneo ya mipakani, wanapata huduma za mawasiliano ya uhakika ili kuboresha maisha yao na kukuza uchumi wa Taifa.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua hali ya mawasiliano mkoani Songwe katika vijiji vya Kapele, Iyendwe, Mpande Kati, na kituo cha forodha cha mpaka wa Tunduma aliyoifanya Oktoba 15, 2025, Bw. Abdulla alisema ni wajibu wa Wizara hiyo ni kuhakikisha changamoto zote za upatikanaji wa mtandao zinatatuliwa kwa haraka ili wananchi waweze kunufaika na fursa za kidijitali.
Ameeleza kuwa, pamoja na changamoto ndogo zilizopo, Tanzania kwa sasa haina tatizo kubwa la mawasiliano kwa sababu maeneo mengi yana minara ya mawasiliano, na kuwaelekeza watoa huduma wote wa simu kushirikiana kutumia minara iliyopo ili kuwezesha mitandao yote kupatikana kwa urahisi katika vijiji vyote.
Ameeleza kuwa Wizara hiyo inaangalia uwezekano wa kuboresha sheria na sera ili kuwezesha mfumo wa “National Roaming”, ambapo mtumiaji wa laini ya mtandao mmoja ataweza kutumia mnara wa mtandao mwingine akiwa ndani ya mipaka ya Tanzania, jambo litakalosaidia kuboresha upatikanaji wa mawasiliano vijijini na maeneo ya pembezoni.
Kwa upande wake, Mhandisi Peter Mwasalyanda, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), alisema mfuko huo unatekeleza mradi mkubwa wa minara 758 unaofadhiliwa na Serikali na ambao umefikia asilimia 98 ya utekelezaji wake.
Amesema UCSAF pia imepanga kuanzisha miradi mipya katika maeneo ya mipakani, mbuga za wanyama na njia kuu za reli za SGR na TAZARA, lengo likiwa ni kuhakikisha huduma za mawasiliano zinapatikana hata katika maeneo yenye umuhimu wa kimkakati kwa maendeleo ya Taifa.