Eleuteri Mangi, Mbarali
Mkuu wa wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya Brigedia Generali Maulid Surumbu amewataka wananchi wa wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya kutumia vyema Kliniki ya Ardhi inayofanyika wilayani humo kujipatia huduma za sekta ya ardhi ikiwemo hati milki za ardhi ili ziweze kuwasiadia katika shughuli zao za kiuchumi.
“Ardhi ikipata thamani unaweza kukopea, huwezi kwenda kukopea ardhi ambayo haina hati, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani alisema kila kipande cha ardhi cha Tanzania ambacho kinamilikiwa na mtanzania, ni muhimu kitambuliwe, kipimwe na apate Hati Miliki ya Ardhi” amesema Brigedia Generali Surumbu.
Akikabidhi hati za umiliki wa ardhi za kielekroniki kwa wananchi wa Kata ya Igurusi Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya Oktoba 18, 2025, Mkuu wa Wilaya hiyo amempongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuiboresha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kutekeleza maajukumu yake kwa kuwapeleka wataalam wake kufanya kazi karibu na wananchi wa Igurusi.
Brigedia Generali Surumbu amesema, zaidi ya viwanja 30,700 vimerasimishwa, hati zimeanza kuandaliwa na kutolewa ambapo kwa sasa huduma za ardhi zimesogezwa kwa wananchi na hivyo kupungunga gharama na muda kwa kuifuata huduma hiyo Wilayani na Mkoani.
Kwa mujibu wa Brigedia Generali Sarumbu, serikali inaendelea kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi hatua inayowarahisishia kupata Hati Miliki za Ardhi wakiwa katika maeneo yao badala ya kusafiri umbali mrefu kwenda kupokea hati hizo Ofisi za Ardhi za Mkoa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ramani kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Joseph Ikorongo amesema wananchi wa Mbarali wamehamasishwa na kuhamasika baada ya kufanyiwa urasimishaji kwa nyakati tofaurti tofauti na zaidi ya wananchi zaidi ya 1000 wameshasikilizwa na kupapa huduma kwenye maeneo ya Igurusi, Rujewa na Ubaruku katika halmashauri ya Mbarali.
“Huduma za Hati za umiliki wa ardhi umerahisishwa ambapo wizara imetengeneza mfumo wa e-Ardhi ambao ukiweka maombi yako ndani ya muda mfupi unapata hati yako ndani ya muda mfupi”. Amesema Bw. Ikorongo.
Gabriel Kamwela na Neema Mkwama ambao ni miongoni mwa wananchi waliopata hati milki za ardhi katika Kliniki ya Ardhi Mbarali wamesema kuwa kupata hati ya ardhi kwa sasa imekuwa rahisi kwa kuwa huduma ya imesogezwa karibu na wananchi jambo walilolieleza limepunguza migogoro ya ardhi isiyo ya lazima.