

Idara ya Uhamiaji nchini imetoa taarifa ikieleza kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Wegesa Heche, alondoka nchini kupitia mpaka wa Sirari, wilayani Tarime, bila kufuata taratibu na kanuni za uhamiaji.
Taarifa ya Idara hiyo imesema tukio hilo lilitokea katika Kituo cha Uhamiaji cha Sirari, mkoani Mara, ambapo Heche alivuka mpaka na kuingia nchini Kenya kinyume na masharti ya Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54.

“Idara ya Uhamiaji inapenda kuujulisha umma kuwa katika Kituo cha Uhamiaji cha Mpaka wa Sirari mkoani Mara, Mheshimiwa John Wegesa Heche, ameondoka nchini kwa kuvuka mpaka na kuingia nchi jirani bila kufuata taratibu na kanuni za uhamiaji zilizoundwa chini ya Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54” imeeleza taarifa hiyo.
Idara hiyo imetoa wito kwa Watanzania na wageni wanaotoka au kuingia nchini kuhakikisha wanafuata taratibu zote za kisheria zinazohusu uingiaji, ukaaji na utokaji wa watu nchini, ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria.