Askofu Mkuu wa Makanisa ya International Evangelism (IEC) Tanzania, Askofu Dkt. Eliudi Issangya akizungumza katika ibada maalumu ya kuliombea Taifa jijini Arusha.
………
Happy Lazaro , Arusha.
Askofu Mkuu wa Makanisa ya International Evangelism (IEC) Tanzania, Askofu Dkt. Eliudi Issangya, amewataka Watanzania kuendelea kuhubiri amani na umoja kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Akizungumza katika ibada maalumu ya kuliombea Taifa, iliyofanyika Makao Makuu ya kanisa hilo Sakila, wilayani Arumeru, Askofu Isangya amesema Watanzania hawapaswi kuruhusu watu wenye nia ovu kuwapandikizia chuki na kuvuruga amani ambayo imekuwa nembo ya Taifa tangu enzi za waasisi wake.
Askofu Issangya amesema kuwa,hivi sasa tunavyoelekea kwenye uchaguzi oktoba 29 ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anahubiri amani na mshikamano ili amani iendelee kutawala na uchaguzi kumalizika kwa amani.
“Ni muhimu kwa kila mtanzania kuiombea nchi kwa imani yake hususani tunapoelekea kipindi.cha uchaguzi na swala la maombi tusiwaachie wachungaji peke yao bali kila.mmoja ahakikishe anasimama kwa nafasi yake.”amesema Askofu Issangya.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake IEC Eunice Sumari amesema wanawake na watoto ndio wanaoumia zaidi pale amani inapovunjika ambapo amesema kwa maana hiyo wameamua kuomba na kuamini kuwa uchaguzi utafanyika kwa amani.
“Jamani kila mmoja wetu anajua kunapokuwepo na uvunjifu wa amani mahali popote wanaoathirika zaidi ni wanawake na watoto hivyo ni jukumu la kila mmoja kuiombea nchi yetu ili.uchaguzi uweze kukamilika kwa amani.”amesema.
Naye Mchungaji wa IEC ‐Julius Kimaro amesema kuwa, kwa sasa hivi kila mmoja anapaswa kuendelea kudumisha amani iliyopo kwa kuomba na kuendelea kuhubiri amani na upendo kwa kila mmoja ili nchi yegu iendelee kubakia salama.
Ibada hiyo iliyohudhuriwa na zaidi ya waumini 1,000 ambapo Askofu Dkt .Issangya amesema makanisa yote ya IEC nchini na nje ya Tanzania yanaendelea na maombi maalum kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa utulivu na heshima, huku akisisitiza kuwa Mungu yuko nyuma ya Watanzania wanaotetea amani.