

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa taasisi za dini kutambua wajibu wa kuendelea kusimama katika nafasi yake ya kuombea taifa, kufundisha imani ya kweli ya Mungu, kukemea maovu katika jamii, kufundisha maadili mema na kuwa kielelezo cha haki na uadilifu.
Makamu wa Rais ametoa wito huo mara baada ya kushiriki Ibada Maalum ya Jubilei ya Miaka 50 ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Pare, iliyofanyika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro. Amesema kwa njia hiyo Kanisa litachangia katika kujenga jamii inayowajibika na yenye uadilifu. Aidha, amesema ni muhimu kuwa wabunifu na kutumia fursa ya maendeleo makubwa ya TEHAMA ikiwemo mitandao ya kijamii katika kuinjilisha na kutoa huduma nyingine muhimu.
Makamu wa Rais amewasihi wazazi, walezi, jamii na Kanisa kwa ujumla kupima faida na madhara ya TEHAMA na kuwajengea uwezo vijana kuhusu matumizi bora ya teknolojia ili yawe matumizi salama na yenye tija. Amesema ni vema kuhimiza mawasiliano ya ana kwa ana kati ya vijana, ikiwemo kuhimiza vijana washiriki vyama vya kufundisha maadili ya dini na mila na desturi njema kupitia michezo, sanaa, shughuli za kijamii na kidini ili kupunguza utegemezi wa kupitiliza kwenye mitandao.
Amesema ulimwengu wa kidijitali umeleta fursa nyingi kwa vijana, Kanisa na Taifa kwa ujumla ikiwemo urahisi wa kujipatia elimu, kupashana habari ikijumuisha kutangaza neno la Mungu na kurahisisha mawasiliano kwa ujumla. Hata hivyo, ulimwengu huo wa kidijitali umeambatana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na hatari kwa vijana kuathirika na maudhui hasi kama unyanyasaji mtandaoni, picha na video chafu, ujumbe wa kuchochea chuki, kuathirika kwa afya ya akili kutokana na utegemezi uliopitiliza kwenye mitandao, muziki masikioni na kupungua kwa mawasiliano ya moja kwa moja miongoni mwa jamii.
MJANE wa ODINGA – WATOTO – WAJUKUU WALIVYOWEKA MASHADA ya MAUA KWENYE KABURI LA RAILA ODINGA….