*Aahidi wananchi kushuhudia mageuzi makubwa kuanzia mwakani
*Aweka wazi mkakati mabasi yaendayo haraka,ujenzi wa Fly Over tatu
Na Said Mwishehe,Michuzi TV
MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM)Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema katika kipindi cha uongozi wake, Serikali imejenga kilometa 94.9 za miundombinu ya barabara katika Jiji la Dar es Salaam ambapo jumla ya sh. trilioni 2.1 zimetumika.
Aidha amesema ujenzi wa awamu zote za mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka(BRT) Serikali inakwenda kukamilisha barabara zote huku ikisimamia uamuzi wa kushirikisha sekta binafsi inapewa nafasi ya kuendesha shughuli za usafirishaji wananchi wa Jiji hilo.
Akizumgumza leo Oktoba 21,2025 mkoa wa Dar es Salaam wakati wa mkutano wake wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu ikiwa ni siku yake ya kwanza kwa mkoa huo ametumia nafasi hiyo kuelezea hatua mbalimbali ambazo Serikali ya awamu ya sita imezichukua kujenga miundombinu ya barabara.
“Tutakapomaliza barabara zote ni fursa muhimu kwa sekta binafsi kupata kazi ya kubeba abiria na kurudisha. Kazi hiyo kwa kiasi kikubwa hatutaki kuifanya Serikali bali sekta binafsi wataingiza mabasi wafanye uendeshaji wa shughuli hizo.
“Tayari tumeshapata watoa huduma kwenye awamu ya kwanza kampuni ya ENG yenye mabasi 177. Awamu ya pili kampuni ya Mofat yenye mabasi 255 na mabasi ya Mofat tayari yameshaingia njiani.
“Kampuni ya YG Link yenye mabasi 166 nayo yatakuja kuingia njia zingine zikimalizika na kampuni ya Metro Link City yenye mabasi 334 nayo itaingia kutoa huduma.”
Akiendelea kueleza mipango ya Serikali katika miaka mitano ijayo ni kwamba wananchi kuanzia Januari mwakani wakazi wa Dar es Salaam watashuhudia mageuzi makubwa katika utoaji huduma za miundombinu ya BRT.
Amesema kwamba mradi wa mabasi ya mwendokasi kwa hatua iliyofikia umeletea sifa Tanzania kimataifa katika uwekezaji ndani ya Jiji la Dar es Salaam.
“Niwahakikishie wakazi wa Kinondoni, Ubungo na Dar es Salaam kwa ujumla. Kwa mageuzi yaliyofanyika kwenye uendeshaji tutalinda sifa hiyo kimataifa na mradi wa BRT utaleta mapinduzi ya usafiri ndani ya jiji.
“Kwa ndugu zetu wenye daladala kipindi hiki tuliweza kukamilisha ujenzi wa stendi pale Mwenge kwa ajili ya wenye daladala. Tunapokwenda mbele tunakwenda kufanya ukarabati kuziboresha stendi za daladala za Kawe, Bunju B na Tegeta Nyuki.”
Mgombea urais Dk.Samia amesema kuwa hatua hiyo itaziwezesha daladala kuwa na maeneo maalum ya kutoa huduma.
Pamoja na hayo pia amesema anatambua changamoto ya uchakavu na kuharibika kwa barabara hasa kutokana na mvua kunyesha ambapo ameahidi katika miaka mitano ijayo serikali yake ikipata ridhaa inakwenda kukamilisha ujenzi wa barabara ambazo zimeanza kujengwa.
Ametaja baadhi ya barabara hizo ni barabara ya Kimara- Mavurunza- Bonyokwa hadi Kinyerezi yenye urefu wa kilometa Saba ambayo inapita katika majimbo matatu ya Segerea, Kibamba na Ubungo.
Pia amesema Serikali itaongeza bajeti ili kujenga barabara nyingine muhimu kwa maendeleo ya maeneo kama zilivyo kwenye kitabu chetu cha Ilani ya mkoa wa Dar es Salaam.
“Miongoni mwa miradi mipya tutakayotekeleza Kinondoni ni upanuzi wa barabara ya Mwaikibaki sehemu ya kilometa 9 kutoka Morocco hadi Kawe na upanuzi wa barabara ya Tegeta- Bagamoyo yenye kilometa 57.”
Mgombea urais Dk.Samia amesema kuwa watakapomaliza kuboresha barabara za ndani za Ubungo pia watakamilisha ujenzi wa barabara ya Kibamba- Mloganzila.
Pia tutajenga barabara za juu katika makutano ya Morocco- Mwenge, magomeni na barabara ya Ali Hassan Mwinyi na United Nation hatua itakayopunguza msongamano na kuongeza ufanisi wa barabara zetu na kukuza shughuli za biashara.
Kwa upande wa maeneo yanayokabiliwa na changamoto ya mafuriko msimu wa mvua, Dk.Samia amesema mradi wa DMDP 2 utakwenda kushughulia changamoto hizo na kuziondoa kabisa.
Amefafanua kwamga kuna maeneo ya Kinondoni ambayo wanakwenda kuyafanyia kazi pamoja na kukamilisha ujenzi wa mifereji kwa lengo la kuondoa kabisa mafuriko katika eneo la Tandale, Magomeni na Makumbusho na kwa Kawe watajenga mitaro mikubwa ya maji ya mvua kuelekea baharini katika maeneo ya Basihaya.