Na Farida Mangube Morogoro
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Mstaafu ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM), Profesa Mussa Juma Assad, amesema hali ya uchumi wa Tanzania imeimarika katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Profesa Assad ameyasema hayo mjini Morogoro katika Kongamano la Kitaaluma la kujadili Utekelezaji wa Uchumi Jumuishi kufikia Dira 2050, lililoandaliwa na Chuo kikuu MUM kwa kushirikiana na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC).
Amesema kwa vigezo vya kiuchumi, Tanzania inaendelea kufanya vizuri ukilinganisha na baadhi ya nchi jirani kama Kenya na Rwanda, ambapo ukuaji wa pato la taifa (GDP) umeendelea kuwa thabiti.
“Kwa jumla, uchumi wa Tanzania umekuwa kwa wastani wa asilimia sita. Pato la Taifa limekuwa likipanda na kushuka kwa uwiano mzuri ukilinganisha na nchi jirani. Kwa hali ya sasa, Watanzania wengi wana uwezo wa kuendesha maisha yao, jambo linaloashiria uimara wa uchumi wetu,” amesema Profesa Assad.
Akizungumzia dhana ya uchumi jumuishi, Profesa Assad meisema ni muhimu serikali na sekta binafsi kushirikiana kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na fursa za kiuchumi, hasa vijana wanaomaliza vyuo vikuu.
Alibainisha kuwa changamoto kubwa siyo ukosefu wa nafasi katika uchumi, bali ni uhaba wa ujuzi miongoni mwa wahitimu. Alipendekeza serikali na sekta binafsi kuandaa kozi za miezi mitatu za kuwajengea wahitimu uwezo wa vitendo.
“Vijana wanaomaliza vyuo wanapaswa kupewa ujuzi wa ziada baada ya kuhitimu. Hii ni kazi ya pamoja kati ya serikali na sekta binafsi ili kuhakikisha wanakuwa na kitu cha kufanya,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa PPPC, Bw. David Kafulila, amesema katika kipindi cha miaka minne cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta mbalimbali za uchumi.
Akitolea mfano sekta ya umwagiliaji amesema imeongezeka kutoka hekta 540,000 mwaka 2021 hadi kufikia hekta milioni moja mwaka 2024. Vilevile, sekta ya madini imeimarika, huku mchango wa wachimbaji wadogo ukipanda kutoka asilimia 20 hadi 40.
“Uamuzi wa Rais Samia wa kuzibadilisha hati za wachimbaji wakubwa na kuwapatia wachimbaji wadogo zaidi ya 2,600 umeongeza ushiriki wa wananchi wa kawaida katika sekta ya madini,” alisema Kafulila.
Aliongeza kuwa katika sekta ya nishati, mtandao wa usafirishaji wa umeme umeongezeka kwa kilomita 2,000 ndani ya miaka minne sawa na ongezeko la asilimia 30 ya kiwango kilichojengwa katika kipindi cha miaka 60 iliyopita.
Naye Mchumi na Mwanazuoni, Dk. Bravious Kahyoza, amesema uwiano kati ya biashara na pato ghafi la taifa umeongezeka kutoka asilimia 27 mwaka 2021 hadi asilimia 43 mwaka 2024, ikionesha kuimarika kwa shughuli za kiuchumi na biashara.
Dk. Kahyoza aliongeza kuwa ajira katika sekta ya umma zimeongezeka kwa kasi, ambapo zaidi ya watumishi 400,000 wameajiriwa katika kipindi cha miaka minne — ongezeko kubwa ukilinganisha na nchi jirani.
“Kenya imeajiri watu 311,000, Uganda 196,000 na Rwanda 20,000, hivyo Tanzania imeongoza kwa kasi ya ajira katika sekta ya umma,” amesema.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe na Mtaalamu wa Ubia wa Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), Moshi Derefa, amesema duniani kote sekta binafsi imekuwa injini muhimu ya maendeleo kupitia ubia wa miradi ya kimkakati.
“Tunapaswa kutumia fursa hii ya ubia si tu ndani ya nchi, bali pia kuvutia wawekezaji kutoka nje wenye teknolojia na uzoefu mkubwa ili kuharakisha maendeleo,” alisema Moshi.