Mkuu wa Chuo cha VETA Furahika, Aliko Mmongele, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuchaguliwa tena kuongoza taifa, sambamba na Makamu wa Rais Dk. Nchimbi, huku akieleza kuwa serikali imeendelea kuonyesha dhamira ya dhati ya kuwawezesha vijana kupitia elimu ya ufundi.
Akizungumza chuoni hapo leo Novemba 6,2025 Jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari Mmongele amesema pongezi hizo zinaenda sambamba na jitihada za serikali kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika kuimarisha elimu ya ufundi stadi nchini, jambo linalosaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.
“Kwa niaba ya uongozi wa VETA Furahika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais na Makamu wake pamoja na Rais wa Zanzibar kwa uongozi bora na sisi Tumejipanga kuunga mkono juhudi zao kwa kuhakikisha vijana wanapata mafunzo yatakayowasaidia kujiajiri,” amesema Mmongele.
Amefafanua kuwa chuo hicho kimeanzisha kozi mpya kadhaa zenye lengo la kuwafikia vijana wengi zaidi, kama ambavyo Rais amekuwa akisisitiza juu ya uwezeshaji wa vijana kiuchumi kupitia stadi za kazi.
Miongoni mwa kozi hizo ni ufundi bomba, upakaji rangi, huduma za chakula (catering), na huduma kwa wateja (customer care), ambazo zimebuniwa kutokana na mahitaji makubwa katika taasisi na sekta mbalimbali.
Aidha, Mongele amesema kozi nyingine mpya ni usomaji wa mita za maji, makarani wa mahesabu, na kozi ya awali ya uhasibu, ambazo zinasimamiwa na Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA).
Akizungumzia sifa za kujiunga na kozi ya uhasibu, amesema mwombaji anatakiwa kuwa amehitimu kidato cha nne na kuwa na ufaulu unaokubalika na NBAA, pamoja na kuwa na msingi wa masomo ya biashara.
“Kozi zote tulizoanzisha zimezingatia uhitaji wa soko la ajira na fursa za kujiajiri. Tunataka kuona vijana wakitoka VETA wakiwa na uwezo wa kujitegemea na kutoa huduma bora katika jamii,” anesisitiza Mmongele.
VETA Furahika pia imesisitiza kuwa kozi hizo zinaendeshwa kwa kutumia mtaala rasmi wa VETA, hivyo wahitimu wake watatambulika kitaifa na kimataifa.
Aidha, Mmongele amesema chuo kimeweka utaratibu wa kozi za muda mfupi na muda mrefu, ili kuwapa nafasi watu wenye ratiba tofauti kujiendeleza bila vikwazo.
Amebainisha kuwa chuo kipo katika hatua za mwisho za kuboresha miundombinu, yake ya kufundishia, ili kuhakikisha mazingira ya kujifunzia yanakuwa bora zaidi.
Kozi hizo zinatarajiwa kuanza rasmi mwezi Novemba na Desemba, ambapo usajili kwa wanafunzi wapya umefunguliwa rasmi na vijana wameaswa kujitokeza ili kujiunga na chuo hicho ambapo mafunzo hayo yanatolewa kwa gharama nafuu huku wengine wakiendelea na ufadhiri wa kupata elimu hiyo bure kama ilivyokuwa taratibu za chuo hicho.








