

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezilaumu baadhi ya taasisi za dini kwa kujiingiza kwenye mkumbo wa masuala ya kisiasa, huku akisisitiza kuwa Tanzania haina dini, bali watu wake wana dini na madhehebu mbalimbali. Amesema hakuna madhehebu yoyote yaliyopewa uwezo wa kutoa matamko yanayoharibu mengine kikatiba na kisheria. Ametaka viongozi wa dini kutojificha nyuma ya majoho na kujaribu kuongoza nchi, akisisitiza kuwa Tanzania itaendeshwa kwa Katiba na sheria.
Amesema kuwa ubora wa dini upo mioyoni mwa waumini na kwamba ndani ya madhehebu kumekuwa na tofauti za matamko yasiyofanya kazi, kwa sababu wanaosimama katika mstari wa haki wanayakataa. Dkt. Samia amesema kuwa Tanzania ni nchi ya amani, umoja na utulivu na hakuna sababu ya kuivuruga kupitia siasa au dini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezungumza na wazee wa Dar es Salaam na kuhutubia taifa katika ukumbi wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, leo Desemba 02, 2025.
Dkt. Samia amesema kuwa serikali itasimama kulinda nchi kwa nguvu zote, na kwamba “yaliyopita si ndwele, tugange yajayo”. Ameongeza kuwa kama madai ni kuhusu Katiba, hakuna aliyekataa kufanya marekebisho, na kwamba tayari aliunda Tume ya Haki Jinai iliyotembelea nchi nzima na kuwasilisha mapendekezo yenye masuala ya muda mfupi, wa kati na mrefu, ambapo asilimia tisini yanaweza kutekelezwa.

Aidha amebainisha kuwa wanasiasa wamekuwa wakifanya harakati kwa njia zinazolenga kuvuruga gurudumu la maisha, licha ya kuwa serikali imefanya kazi kubwa katika miaka ya 2020 hadi 2023 kwa kuzungumza na wananchi kupitia njia mbalimbali. Dkt. Samia amesema kuwa baadhi ya watu waliomba kukutana naye na aliwapokea, akizungumza nao. Ameeleza kuwa aliwasaidia kwa kuwapa fedha ili waendelee na maisha, huku akiwaambia wenye kesi kuja kuzungumza.
Amesema kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakimkashifu baada ya kuwapa msaada, jambo ambalo amesema kuwa si tabia ya Watanzania. Dkt. Samia ameongeza kuwa alitoa fursa kwa vijana kufanya shughuli zao za kisiasa, lakini amesisitiza kuwa siasa si kufanana, kubebana au kuharibu, bali ni usalama na uungwana. Amesema kuwa siasa zinazovuruga nchi si siasa sahihi.
Aidha amebainisha kuwa madai yaliyotolewa na chama fulani cha siasa hayakupaswa kudaiwa kwa njia walizotumia, na hakukuwa na masharti ya kukaa meza moja mazungumzo ili warudi kwenye TANU.

Kwa upande wa vijana, Dkt. Samia amesema kuwa vijana wengi waliingizwa barabarani bila kuelewa wimbo waliokuwa wakiimba, na kujiingiza katika vurugu kwa madai ya ugumu wa maisha. Ameeleza kuwa ugumu wa maisha unapaswa kupimwa kwa tafiti mbalimbali ndani na nje ya Afrika, na kwamba wengine walioingia barabarani hawakuwa na ugumu huo bali sababu binafsi. Amesema serikali imejifunza kuwa vijana wengi hawana elimu ya uzalendo na kwamba wizara ya vijana itashughulikia vijana kwa upeo mpana zaidi.
Amesema kuwa serikali imefanya kazi kubwa katika awamu ya sita, ikiwemo kuboresha huduma za afya, elimu na uchumi, na kwamba kama mtu hampendi kiongozi aliyepo, hakuna sababu ya kuvuruga nchi. Dkt. Samia amesema kuwa sumu za chuki zinazotolewa kupitia dini na siasa zinapaswa kuepukwa, kwani chuki ya dini hujenga madhara makubwa moyoni.

Aidha amebainisha kuwa viongozi wa dini wanapaswa kusimama katika mstari sahihi, kwa kuwa mamlaka yote yametoka kwa Mungu, bila kujali kama kiongozi ni mwanamke au mwanamume. Amesema kuwa hakuna kitabu cha dini kilichoelekeza kuvuruga nchi kwa misingi ya kidini.


The post Rais Samia: Baadhi ya Taasisi za Dini Zinajiingiza Kwenye Siasa appeared first on Global Publishers.





