CAIRO: KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Miguel Gamondi, amesema maandalizi ya kuelekea Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) za Morocco 2025 yamejaa dhamira moja kubwa—kuiwakilisha Tanzania kwa heshima, nidhamu na ari ya kupambana.
Akizungumza katika kikao cha tathmini ya maandalizi, Gamondi alisisitiza kuwa anataka kuona Taifa Stars inaingia AFCON kama timu iliyokomaa, yenye umoja na inayobeba sura halisi ya Watanzania.
“Hii si safari ya kutafuta matokeo tu. Ni safari ya kuonesha namna gani tunathamini bendera yetu na taswira ya soka la Tanzania. Tunahitaji kuonesha moyo, kujitoa na nidhamu ya juu,” alisema Gamondi ambaye yuko Yuko nchini Misri na Stars kwa ajili ya fainali hizo zitakazofanyika Desemba 21 hadi Januari 18, mwaka huu.
Gamondi alikiri kuwa kundi walilopangwa si rahisi, lakini akabainisha kuwa kiwango cha maandalizi kilichopangwa kinatosha kupambana na timu yoyote.
“Ndiyo, kundi letu lina ushindani mkubwa… lakini hakuna kisichowezekana kwenye mpira. Tunajiandaa kimwili, kiufundi na kisaikolojia ili kuingia uwanjani bila hofu,” alisema.

Kocha huyo amesisitiza umuhimu wa wachezaji kuwa na fikra chanya na kuamini katika uwezo wao, akisema michezo ya AFCON inahitaji zaidi ya ufundi uwanjani—inahitaji ujasiri na uthubutu.
Amesema kipindi hiki ni cha kujenga zaidi umoja, sababu AFCON ni mashindano ambayo yanahitaji timu kuwa kitu kimoja ndani na nje ya uwanja.
Katika ujumbe wake kwa Watanzania, Gamondi amesema sapoti ya mashabiki ina mchango mkubwa kwa morali na utendaji wa timu:
“Tunajua Watanzania wanapenda mpira. Ni matumaini yangu wataendelea kutusapoti. Tunahitaji hisia zao, nguvu zao na imani yao. Inapokuwa nyuma ya timu, inaongeza ari ya kupambana,” alisema.
Gamondi ameahidi kuendelea kuboresha maandalizi na kuhakikisha kikosi kinakuwa tayari kufanya historia.
The post Gamondi: Tutaingia Afcon kama timu iliyokomaa first appeared on SpotiLEO.






