

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemtaja marehemu Jenista Mhagama kuwa kiongozi jasiri, mlezi wa wengi na nguzo muhimu ya matumaini kwa wanawake na vijana, aliyetoa mchango wa kipekee katika Bunge, Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza leo Desemba 13, 2025 katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kiwanja cha Ndege jijini Dodoma, Rais Samia amesema ni vigumu kupata maneno ya kuelezea msiba mzito wa kiongozi aliyegusa maisha ya watu wengi kama marehemu Mhagama, akibainisha kuwa taifa limepoteza mtumishi wa umma aliyekuwa mfano wa uadilifu, nidhamu na hofu ya Mungu.

Rais Samia amewashukuru viongozi wa dini kwa maombi na misa tangu kutokea kwa msiba huo hadi siku ya kuuaga mwili wa marehemu, pamoja na watu wote walioshiriki kwa namna mbalimbali kushughulikia msiba na kumsitiri marehemu kwa heshima kubwa.
Akizungumzia maisha ya marehemu, Rais Samia amesema Jenista Mhagama alikuwa kiongozi aliyesimama imara kutetea haki, maendeleo na usawa wa watu aliowaongoza, si tu katika jimbo lake la Peramiho bali pia katika ngazi ya taifa. Amesema uongozi wake uliwapa matumaini makubwa wanawake na vijana, huku akionesha mfano wa uongozi uliotawaliwa na misingi ya maadili na hofu ya Mungu.



The post Rais Samia: Jenista Mhagama Alikuwa Kiongozi Jasiri na Nguzo ya Matumaini kwa Wanawake – Video appeared first on Global Publishers.







