NA DENIS MLOWE, IRINGA
MBUNGE wa Iringa Mjini, Mhe. Fadhili Ngajilo, ameongoza hafla ya kufunga bonanza la michezo lililofanyika mjini Iringa, ambapo amesisitiza umuhimu wa matamasha katika kuleta hamasa na kuhuisha shughuli za kijamii ndani ya mji.
Akizungumza kama mgeni rasmi, Mhe. Ngajilo aliwashukuru wananchi wote waliojitokeza kushiriki na kuhudhuria bonanza hilo, akisema uwepo wao ni uthibitisho wa mapenzi makubwa kwa michezo na maendeleo ya Iringa.
Mbunge huyo alikiri kuwa hatua zake za awali katika kuanzisha bonanza hilo zilikuwa kama majaribio, lakini mafanikio yaliyoonekana yamempa moyo wa kuweka mikakati ya kufanya matamasha makubwa zaidi siku zijazo.
“Mji uchangamke, mji usilale,” alisema, akihimiza ongezeko la shughuli za burudani na michezo ili kukuza umoja, afya na uchumi wa jiji la Iringa.
Mhe. Ngajilo pia aliipongeza kamati ya maandalizi kwa kazi nzuri na kwa kuhakikisha bonanza hilo linafana na kuwafikia wananchi wengi kutoka maeneo mbalimbali.
Alisema amefurahishwa sana kuona ushiriki mkubwa wa vijana, timu za michezo na wasanii, jambo linaloonyesha kiu ya jamii kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii.
Mbunge huyo alisisitiza umuhimu wa mshikamano na umoja, akiwataka wakazi wa Iringa kuendelea kupendana na kushirikiana katika shughuli zote za kijamii na maendeleo.
“Iringa yetu maisha yetu, na maisha yetu Iringa yetu,” alisisitiza, akitoa wito wa kudumisha uzalendo na kuwajali vijana ambao ni nguzo ya maendeleo ya mkoa.
Katika hotuba yake, Mhe. Ngajilo aliahidi kuwa serikali na uongozi wake wataendelea kufanya juhudi za dhati kuboresha mazingira na miundombinu ya michezo katika mkoa wa Iringa.
Akitaja baadhi ya miradi inayoendelea, alisema kuwa shilingi milioni 30 tayari imetengwa kwa ajili ya ukarabati na uboreshaji wa Uwanja wa Mlandege, ikiwemo kupanda nyasi na kutengeneza viwanja vya ziada.
Mbali na maboresho ya viwanja, aliahidi pia vifaa vya michezo kwa timu, pamoja na kutoa nafasi kubwa kwa wasanii kupata promo ili kuendeleza vipaji vyao na kukuza tasnia ya muziki mkoani Iringa.
Mwisho, mbunge huyo aliwahakikishia wananchi kuwa uongozi wake utashirikiana na wadau wote katika kuinua michezo yote, akiwataka vijana kutumia fursa hizo kuimarisha vipaji vyao na kutangaza vyema Iringa.






