MSTAHIKI Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Iranghe akizungumza kwenye halfa hiyo katika.soko la mitumba Mbauda
Happy Lazaro,Arusha
Arusha .MSTAHIKI Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Iranghe, ametoa masaa matatu kuondolewa kwa mrundikano wa taka katika soko la mbauda huku akisisitiza kuwa atarejea binafsi kukagua utekelezaji wa agizo hilo kama umefanyika.
Ameyasema hayo leo wakati wa ziara ya kampeni ya “Ng’arisha Jiji” katika Soko la Mitumba Mbauda, kata ya Sombetini.
Meya Iranghe amesema suala la usafi si mjadala wa kisiasa bali ni wajibu wa kiutendaji, akionya kuwa hatasita kuchukua hatua kali dhidi ya viongozi na watendaji wanaoshindwa kutimiza majukumu yao.
“Natoa maelekezo kontena la uchafu liondolewe ndani ya masaa matatu. Nikirudi hapa nisilikute,” amesisitiza Meya.
Iranghe alionekana kukerwa na harufu kali na mrundikano wa taka ngumu zilizokuwa zimejaa kwenye kontena la soko hilo, hali ambayo wafanyabiashara walieleza kuwa taka hizo hukaa kwa zaidi ya wiki mbili, kunyeshewa na mvua na kuhatarisha afya zao kutokana na uwezekano wa magonjwa ya mlipuko.
Aidha Meya amesema kuwa ,haiwezekani mapambano ya usafi wa mazingira yakabaki kuwa jukumu lake pekee, huku baadhi ya watendaji waliokabidhiwa dhamana hiyo wakishindwa kumuunga mkono kwa vitendo.
“Nilipokabidhiwa uongozi, Jiji la Arusha lilikuwa likishika nafasi ya mwisho kwa uchafu, lakini kupitia juhudi na msimamo wake, kwa sasa limepiga hatua na kufikia nafasi ya pili kwa usafi, hatua ambayo haipaswi kurudishwa nyuma kwa uzembe wa baadhi ya wahusika na mimi.nitakuwa bega kwa bega kukemea vikali tabia hiyo .”amesema Meya .
“Siwezi kupambana peke yangu. Nimekuta Jiji la Arusha likiwa la mwisho kwa uchafu, sasa hivi tumepanda hadi nafasi ya pili kwa usafi. Haiwezekani katika mapambano haya nibaki mwenyewe huku wengine wakidai natafuta umaarufu. Hapa hakuna siasa, hii ni kazi,” amesema Iranghe.
Amesisitiza kuwa dhamana aliyopewa ni ya kuwatumikia wananchi, si kujijenga kisiasa, akionya kuwa atawawajibisha wote watakaokwaza juhudi za kufanya Arusha kuwa jiji safi na salama kiafya.
“Hii ni kazi mmenipa, lazima niwatumikie wananchi. Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, usipowajibika awamu hii, nitakuwajibisha,” alionya kwa msisitizo.
Akiendelea kutoa maelekezo, Meya aliagiza kuitishwa kwa kikao cha maafisa tarafa na mawakala wa ukusanyaji taka, ili kubaini sababu za uzembe katika usimamizi wa usafi wa mazingira jijini.
Pia alimuelekeza Katibu wa Soko kusimamia kikamilifu kanuni za usafi, akitangaza kuwa ni marufuku kufanya biashara bila kufanya usafi, na kwamba baada ya shughuli za biashara, usafi ufanyike mara moja.
Aidha, Iranghe alielekeza utozwaji wa faini kwa wote wanaokiuka sheria za usafi uendelee bila kusita, na kwa waendelezao ukaidi wachukuliwe hatua kali ikiwemo kuondolewa sokoni, ili kupisha wafanyabiashara wanaoheshimu sheria na kanuni zilizopo.
“Soko hili nalifahamu wanalipa ushuru. Nawataka Mkurugenzi na madiwani warudi wakae kuangalia namna ushuru huo utatumika kuboresha soko hili au kujenga soko jipya la kisasa,” amesema.
Aidha Meya amewaagiza madiwani wote wa Jiji la Arusha kusimamia ipasavyo suala la usafi katika kata zao, kurejesha kwa nguvu utozwaji wa faini kwa wazalishaji na wasambazaji wa uchafu, na kuhakikisha kuwa kabla ya kufungua biashara—usafi ufanyike kwanza, ili kulinda afya za wananchi na taswira ya Jiji la
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Sombetini, Godfrey Kitomari, amesema changamoto kubwa ni kontena la kukusanyia taka ambalo limekuwa likizidiwa na uchafu na kuchelewa kuondolewa, hali inayosababisha harufu kali kuenea katika soko zima la mitumba Mbauda.
Amewahimiza wafanyabiashara na wananchi wa kata hiyo kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika shughuli za usafi ili kuunga mkono sera ya mazingira ya Serikali.






