DAR ES SALAAM:MKE wa Mkubwa Fella maarufu kama Sweet Fella amevunja ukimya na kuwajibu wanaomchokonoa kupitia mitandao ya kijamii, akidai kuwa tayari amechukua hatua dhidi yao na athari zake zinaonekana hadi sasa.
Kupitia Instagram Story yake, Sweet Fella amesema kuwa licha ya kumpiga “moja tu”, tayari baadhi ya watu wameanza kuonekana kupoteza mwelekeo, huku akionya kuwa endapo atachukua hatua kwa mara ya pili, basi huenda wasiweze kuzungumza kwa muda mrefu.
“Naona mnaanza kunichokonoa, nimewapiga moja tu mpaka leo mnaweweseka. Wiki ya pili hii, nikija kwa mara ya pili si mtaongea mwezi. Acheni kujishitukia ndugu. Kasikilizeni klipu vizuri, labda masikio yenu ni mazito, zidisheni sauti mpaka mwisho,” ameandika Sweet Fella.
Katika hatua nyingine, Don Fumbwe ametoa ufafanuzi mzito kuhusu mchango wa Diamond Platnumz katika matibabu ya Mkubwa Fella, akisema kuwa mbali na gharama za matibabu ya Tanzania na India zilizofikia zaidi ya Sh milioni 200, Diamond alimpa mke wa Mkubwa Fella Dola 20,000 za Marekani (zaidi ya Sh milioni 50) kama msaada wa ziada nje ya matibabu.
Aidha, Don Fumbwe amesema baada ya kurejea kutoka India, Diamond alitoa Sh milioni 20 mara mbili na Sh milioni 15 mara moja, jumla ya Sh milioni 55, kwa nyakati tofauti, kwa ajili ya matibabu ya kliniki na uangalizi wa baada ya matibabu makubwa.
Ameongeza kuwa kulikuwepo na malalamiko kutoka kwa familia kwamba Diamond anazuia wengine kutoa msaada, hali iliyomfanya msanii huyo ajiondoe taratibu ili kuwapa nafasi watu wengine kusaidia.
“Diamond akajisikia vibaya ili watu wengine wapate nafasi, kwa sababu tayari alikuwa ameshafanya mambo makubwa ya kimatibabu,” amesema Don Fumbwe.
The post Mke wa Mkubwa Fella awajibu wakosoaji: first appeared on SpotiLEO.





