Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza Januari 13, 2026, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) uliofanyika Makao Makuu ya Mahakama, Dodoma.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, George Mcheche Masaju akizungumza katika mkutano huo uliofunguliwa Januari 13, 2026 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Makao Mkuu ya Mahamkama jijini Dodoma
……….
Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza umuhimu wa uhuru wa Mahakama na jukumu la majaji na mahakimu katika kuhakikisha haki inapatikana kwa wote. Ameyasema hayo Januari 13, 2026, wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) uliofanyika Makao Makuu ya Mahakama, Dodoma.
Aidha, Rais Samia amebainisha kuwa Mahakama huru yenye uadilifu na uwezo ni nguzo muhimu ya utawala bora na msingi wa maendeleo endelevu ya Taifa. Vilevile, amewapongeza majaji na mahakimu kwa kazi kubwa wanayofanya kwa wananchi, akibainisha kuwa majukumu yao ni mazito na yanahitaji weledi, uadilifu, uvumilivu, busara na ujasiri wa kutetea haki bila upendeleo wala rushwa.
Pia, Rais Samia ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha Mahakama, ikiwemo kuboresha miundombinu, kuongeza rasilimali watu, kuboresha maslahi ya watumishi na kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Hatua hizo zinalenga kuharakisha utoaji wa haki.
Aidha, Rais Samia amebainisha kuwa Mahakama ina nafasi muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025–2050, kwani sehemu kubwa ya utekelezaji wa dira hiyo inategemea ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi. Ameongeza kuwa migogoro ya kibiashara, kodi na mikataba ya uwekezaji itahitaji Mahakama kusimama imara katika kulinda haki za wananchi na maslahi ya Taifa.
Akizungumzia suala la bajeti na maslahi ya majaji na mahakimu, Rais Samia ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mishahara na mazingira ya kazi kadri uchumi wa nchi unavyoruhusu. Aidha, amebainisha kuwa changamoto zilizowasilishwa, ikiwemo migogoro ya ardhi na mapendekezo ya mabadiliko ya sheria, zimepokelewa na Serikali na zitatekelezwa kadri rasilimali zitakavyopatikana.
Pia, Rais Samia amesisitiza kuwa majaji na mahakimu wana wajibu wa kusimamia haki kwa kuzingatia Katiba, sheria na maadili bila woga, upendeleo au chuki, akibainisha kuwa ni jukumu lao kulinda amani, usalama na utulivu wa Taifa.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, George Mcheche Masaju, amebainisha kuwa uwepo wa Rais Samia katika mkutano huo unaonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kulinda uhuru wa Mahakama na kuimarisha utoaji wa haki nchini. Aidha, Jaji Mkuu amesema hatua zilizochukuliwa kuboresha majengo, vitendea kazi, rasilimali watu na TEHAMA zitaongeza ufanisi wa Mahakama katika utoaji wa haki kwa wananchi.
Mkutano Mkuu wa TMJA 2026 unahusisha majaji na mahakimu kutoka ngazi zote nchini, ukilenga kujadili masuala ya kitaaluma, kimaadili na kiutumishi kwa lengo la kuimarisha mhimili wa Mahakama na mchango wake katika maendeleo ya Taifa.





