Januari 31,2026
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI )Profesa Riziki Shemdoe, ametoa maagizo kwa mikoa Tanzania Bara kuanza kujipanga mapema kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya elimu, ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi wa Kidato cha Kwanza ifikapo mwaka 2028.
Amesema kuanzia mwaka 2028, wanafunzi wa Darasa la Sita na la Saba watajiunga na Kidato cha kwanza kufuatia mabadiliko ya mitaala, hivyo halmashauri na mikoa zinapaswa kuanza kutenga bajeti mapema ili kuepuka changamoto zitakazoweza kujitokeza baadaye.
Ametoa maagizo hayo Januari 31, 2026, wakati wa ziara ya siku moja wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, ambapo pia ameelekeza watumishi wapya wa sekta ya Afya na Elimu waliopokelewa nchini kupangiwa vituo kulingana na mahitaji halisi, hasa katika shule zenye uhaba wa walimu na vituo vipya vya afya visivyo na watumishi wa kutosha.
Aidha, Prof. Shemdoe amesisitiza viongozi wa wilaya na mikoa kutenga muda wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi na kuwataka Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwapa taarifa Waheshimiwa Wabunge kuhusu mapokezi ya fedha na utekelezaji wa miradi katika maeneo yao.
Katika ziara hiyo, Prof. Shemdoe amekagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari Sheshila Ladwa, Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Shule ya Sekondari Matimbwa, Jengo la Watoto Njiti katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo na kusalimia wananchi wa Mapinga na baadaye kuzungumza na watumishi wa umma katika Ukumbi wa Chuo cha TASUBA, Bagamoyo.
Akitoa salamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema mkoa huo umeanza utekelezaji wa mpango wa ufundishaji kwa njia ya mtandao (Smart Class), ambapo kila halmashauri inatakiwa kuanza na angalau shule moja kwa kununua vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya mpango huo.
Kunenge ameongeza , katika utekelezaji wa ahadi za siku 100, Mkoa wa Pwani tayari una viwanda sita vilivyo katika hatua mbalimbali, ambapo viwanda vitatu tayari vimeanza ujenzi.






