Nahodha wa Simba, Shomari Kapombe aibua gumzo baada ya kushindwa kuweka wazi maana halisi ya staili yake mpya ya kushangilia mabao, inayohusisha kutembea kama mzee anayesaidiwa na mkongojo, akisema ni staili atakayoendelea nayo kila anapofunga.
Kapombe alionekana kwa mara ya kwanza akitumia staili hiyo katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance de Tunis, uliochezwa hivi karibuni, ambapo alishangilia kwa namna iliyowaacha wengi njia panda.
Katika kushangilia huko, beki huyo wa kulia alionekana akishika mfano mkongojo, ishara iliyozua tafsiri tofauti miongoni mwa mashabiki, huku baadhi wakiamini ni ujumbe maalum aliokusudia kuuwasilisha.
Akizungumza kuhusu staili hiyo, Kapombe amesema ameamua kuitumia kama sehemu ya kujipa motisha binafsi, hasa kutokana na maneno ya kubezwa anayopata kutoka kwa baadhi ya watu.
Nahodha huyo wa Simba aliongeza kuwa kila atakapopata nafasi ya kufunga, ataendelea kushangilia kwa staili hiyo ya kutembea kama mzee, kama njia ya kuwajibu wanaomdharau au kumuita mzee.
“Hivi sasa nawaacha wanaoelewa maana yake waendelee kuelewa kwa njia yao, lakini hapo baadaye nitaweka wazi sababu hasa zilizonifanya nichague hii staili,” amesema Kapombe.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, staili hiyo ya Kapombe inalenga kuwapa majibu wale wanaomkosoa na kumbeza, huku akionyesha kuwa bado ana nguvu, ari na ‘damu inayochemka’ ndani ya uwanja.
Source SIMBA WABAKI NJIA PANDA, TAFSIRI TOFAUTI YA KAPOMBE at Soka La Bongo.








