*Yapata kiasi cha Sh.bilioni 63.27 ikilinganishwa na Sh.bilioni 30 zilizopangwa kupatikana
Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA
ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA) imesema kuwa mauzo ya hatifungani
ya benki ya Azania yamepata mafanikio ya asilimia 210.9,ambapo kiasi cha
shilingi bilioni 63.27 kimepatikana ikilinganishwa na shilingi bilioni
30 zilizopangwa kupatikana.
Aidha, asilimia 70 ya mauzo ya
hatifungani imetoka kwa wawekezaji mmoja mmoja yaani Retail Investors na
asilimia 30 imetoka kwa Kampuni na Taasisi. Kati ya wawekezaji wote
walioshiriki, asilimia 98.4 ni wawekezaji wa ndani na asilimia 1.6 ni
wawekezaji wa kigeni.
Hayo yamesemwa leo Januari 24,mwaka 2025 na
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA),
CPA. Nicodemus Mkama wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa toleo la kwanza
la hatifungani ya Benki ya Azania(Azania Bond Yangu) katika Soko la
Hisa la Dar es Saaam.
“Leo sekta ya masoko ya mitaji ina furaha
kubwa kwa kuwa Mgeni Rasmi wetu Waziri wa Fedha Dk.Mwigulu Nchemba
umewezesha kufikia mafanikio ya hatifungani hii kwa kiwango cha hali ya
juu na kwa ufanisi mkubwa, kwani ulikuwa mgeni rasmi katika hafla ya
uzinduzi wa mauzo ya hatifungani hiyo iliyofanyika Novemba, 4 mwaka
2024.
“Na leo wewe ni Mgeni Rasmi katika hafla ya kuorodhesha
hatifungani hii katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE).Tunakushukuru
kwa kuwezesha mafanikio haya makubwa kwa kiwango cha hali ya juu.
“Mafanikio
haya yana maana kubwa katika ustawi na maendeleo ya sekta ya fedha,
kwani inaonesha imani waliyonayo wawekezaji kwa benki ya Azania na
masoko ya mitaji, ambapo masoko ya mitaji hapa nchini yamekuwa na bidhaa
mpya na bunifu zinazokidhi matakwa ya wawekezaji wa ndani na wa
kimataifa,”amesema CPA.Mkam
Ameongeza
kuwa mafanikio hayo ni uthibitisho wa mazingira wezeshi ya kisera,
kisheria na kiutendaji yanayotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini
ya Uongozi madhubuti wa Rais Dkt. Samia Saluhu Hassan,akisaidiwa na
Waziri wa Fedha kuisimamia Sekta ya Fedha.
Amefafanua baadhi ya
mazingira hayo wezeshi ni uwepo wa vivutio vya kuwekeza katika masoko ya
mitaji, ambapo katika mwaka wa Fedha 2021/2022, kupitia Sheria ya Fedha
uliwezesha kuidhinishwa maombi ya kuweka kivutio cha kuwekeza katika
hatifungani za kampuni na taasisi kwa kuondoa kodi ya zuio kwenye faida
ya hatifungani za kampuni na taasisi. Hiyo imekuwa mojawapo ya vivutio
kwa wawekezaji kwenye hatifungani ya Benki ya Azania.
Pia uwepo
wa punguzo la kiwango cha chini chaushiriki katika uwekezaji kwenye
hatifungani ya benki ya Azania, kilichoidhinishwa na CMSA kutoka
shilingi milioni moja hadi Sh. 500,000). Punguzo hilo limewezesha
ushiriki wa wawekezaji wengi, ikiwa ni pamoja na wawekezaji mmoja
mmoja(retail investors) ikijumuisha makundi maalum, hususan vijana na
wanawake.
Aidha ubunifu wa kuweka malipo ya riba ya hatifungani
kwa wawekezaji kufanyika mara nne kwa mwaka badala ya mara mbili, ambapo
CMSA imeidhinisha wawekezajikulipwa riba kila baada ya miezi mitatu
(3)badala ya miezi sita (6).
“Hatua hii pia imekuwa kivutio
kikubwa kwa wawekezaji, kwani inawezesha wawekezaji kuwa na ukwasi na
kipato katika muda mfupi, na hivyo kuwezakukidhi mahitaji mengine.Poa
elimu ya uwekezaji inayotolewa kwa umma na wadau katika sekta ya fedha
kuhusu fursa na faida zinazopatikana katika masoko ya mitaji.”
CPA.Mkama
amesema mafanikio ya hatifungani ya benki ya Azania ni hatua muhimu
katika utekelezaji wa Mkakati wa Serikali wa kuwa na njia mbadala za
upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kuendeleza na kukuza
biashara; na kugharamia shughuli za maendeleo katika sekta ya umma na
binafsi.
Amefafanua kuwa kama ilivyoelezwa kwenye taarifa ya
Mkurugenzi Mtendaji; na kwenye Waraka wa Matarajio wa benki ya Azania,
Fedha kupitia mauzo ya hatifungani hii zitatumika kutekeleza mkakati wa
benki ya Azania wa kukuza na kuendeleza biashara, ikiwa ni pamoja na
kutoa mikopo kwa kampuni ndogo na za kati za ujasiriamali (SMEs) ambazo
zinatoa huduma katika sekta za uchumi; na ambazo zinatoa huduma kwa
makundi ya wanawake na vijana.
Hivyo kwa mantiki hiyo hatifungani
hiyo inawezesha utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Kuwezesha
Upatikanaji wa Rasilimali Fedha kwa Kampuni Ndogo na za Kati za
Ujasiriamali 2023/24 – 2028/29,
Ambapo kampuni ndogo na za kati
za ujasiriamali (SMEs)ambazo ni kichocheo na kiungo muhimu katika sekta
ya kilimo, viwanda na biashara zitafaidika na hivyo kuchagiza maendeleo
na ustawi wa sekta ya fedha na uchumi kwa ujumla hapa nchini.
“Tunawapongeza
sana Bodi na Menejimenti ya benki ya Azania kwa kuchukua hatua hii
ambayo ni kichocheo muhimukatika maendeleo ya uchumi. Kuorodheshwa kwa
Hatifungani ya Benki ya Azania katika Soko la Hisa leo hii, kunaongeza
thamani ya uwekezaji katika Hatifungani za Kampuni na Taasisi kwa
asilimia 8.17 na kufikia Shilingi bilioni 837.31, kutoka Shilingi
bilioni 774.04.
“Hivyo, tuna kila sababu ya kuipongeza Bodi na
Uongozi wa benki ya Azania; pamoja na taasisi na wataalamu wote
walioshiriki katika kuwezesha mafanikio haya. Ninatambua kwamba, kazi
hiyo haikuwa ndogo na rahisi lakini mmeweza kufanya kazi yenu vizuri na
hivyo kufanikisha hatua hii kwa weledi na kwa ufanisi mkubwa.
“Natoa
mwito kwa Benki zingine za Biashara, Taasisi za Fedha, kampuni binafsi
na Mashirika ya Umma kutumia fursa zilizopo katika masoko ya mitaji kama
ambavyo Benki ya Azania imetumia fursa ya kupata shilingi bilioni 63.27
kupitia masoko ya mitaji kwa kuuza hatifungani.
“Mamlaka ya
Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA)itaendelea kuweka mazingira wezeshi na
shirikishi kwa ajili ya kuwezesha taasisi katika sekta ya umma na
binafsi kupata rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mikakati
yenye lengo la kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya watu.”
Waziri
wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akigonga kengele
kuashiria kuorodhoreshwa rasmi kwa Hati Fungani ya Benki ya Azania
ijulikanayo kama Bondi Yangu, katika Soko la Hisa la Dar es Salaam
(DSE), Hafla iliyofanyika katika Ofisi za DSE, jijini Dar es Salaam,
ambapo pamoja na mambo mengine aliziasa taasisi zingine kuiga mfano wa
Azania Bank wa kujiorodhesha kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam na
kutoa fursa kwa wananchi kushiriki kukuza uchumi wao binafsi na uchumi
wa nchi kwa njia za kidijitali.
mbele ya wageni waalikwa wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa toleo la
kwanza la hatifungani ya Benki ya Azania (Azania Bond Yangu) katika Soko
la Hisa la Dar es Saaam leo. Hafla hiyo imefanyika leo katika Ofisi za DSE, jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA), CPA.
Nicodemus Mkama akizungumza mbele ya wageni waalikwa wakati wa hafla ya
kuorodheshwa kwa toleo la kwanza la hatifungani ya Benki ya Azania
(Azania Bond Yangu) katika Soko la Hisa la Dar es Saaam leo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Azania Bank, Esther Mang’enya akizungumza
mbele ya wageni waalikwa wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa toleo la
kwanza la hatifungani ya Benki ya Azania (Azania Bond Yangu) katika Soko
la Hisa la Dar es Saaam leo.