Na Pamela Mollel,MOSHI
MFANYABIASHARA wa Mjini Moshi,Novita Shirima(49) Mkazi wa Katanini ,amefikishwa mahakama ya hakimu Mkazi Moshi , akikabiliwa na mashtaka 6 ya uhujumu uchumi ikiwemo kuzalisha pombe kali bandia aina ya Kvant,Konyagi na Hightlife akitumia kemikali aina ya Ethonol kinyume cha sheria ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya.
Mwingine aliyefikishwa katika mahakama hiyo akikabiliwa na kosa moja la kukutwa na kemikali hiyo aina ya Ethanol lita 90 ni dereva Bajaj Justine Mbise mkazi wa Boma Mbuzi mjini humo.
Akisoma mashtaka hayo jana mbele ya hakimu,Ruth Mkisi wa mahakama hiyo wakili wa serikali,Frank Wambura alisema kuwa mtuhumiwa huyo pamoja na dereva Bajaji,Justine Mbise(29) Mkazi wa Boma Mbuzi Mkoani Kilimanjaro walitenda makosa hayo oktoba 10,2024 katika maeneo tofauti ya Changbay na Katanini katika manispaa ya mji wa Moshi.
Alifafanua kwamba mshtakiwa namba moja Novita Shirima Mkazi wa Katanini anashtakiwa kwa makosa sita ya kujihusisha na Kemikali kinyume cha sheria ya kupambana na dawa za kulevya.Ambapo mnamo oktoba ,10 2024 katika eneo la Katanini mjini Moshi alikutwa na lita 310.9 ya Kemikali aina Ethanol inayodaiwa kutumika katika mchakato wa kutengeneza pombe kali kinyume cha sheria .
Kosa lingine la mshtakiwa huyo ,Novita Shirima ilidaiwa kuwa mnamo oktoba 10,2024 katika eneo la Katanini manispaa ya Moshi alikutwa na Stamps za TRA kinyume cha sheria.
Akisoma kosa la nne wakili wa serikal alidai kuwa mshtakiwa wa kwanza Novita Shirima , mnamo tarehe 10,oktoba 2024,katika eneo la Katanini alikutwa akitumia Stamps za TRA kuweka kwenye chupa akifoji bidhaa ya K vant.
Aidha kosa la tano kwa mshtakiwa namba moja ,ilidaiwa kuwa mnamo tarehe 10,oktoba ,2024,katika eneo la Katanini ,alikutwa akitumia alama ya biashara kwa kufoji chupa 42 zenye ujazo wa Milimita 750 ,kuonesha kuwa bidhaa hiyo imezalishwa na K Vant.
Kosa la sita la mshtakiwa namba moja Novita Shirima ,ilidaiwa kuwa mnamo oktoba 10,2024 katika eneo la Katanini alikutwa na alama ya bidhaa ya biashara aina ya Konyagi chupa 144 zenye ujazo wa milimita 750 kuonesha kuwa bidhaa hiyo ni ya Konyagi.
Akisoma kosa la saba kwa mshtakiwa huyo namba moja Wambura alisema mnamo tarehe 10,0ktoba,2024,mshtakiwa huyo alikutwa akitumia alama ya biashara isivyo sahihi chupa 182 zenye ujazo wa milimita 200 za kampuni ya Highlife kinyume cha sheria.
Wakili wa serikali alidai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na hakimu Mkisi aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 5,Mwaka huu itakapo kuja tena kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu alidai kuwa dhamana kwa washtakiwa wote wawili ipo wazi kwa masharti kwamba kila mmoja awe na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa serikali wenye kudhamini bondi ya sh,milioni 10 kila mmoja, pia kila mshtakiwa aweke dhamana ya kiwanja chenye thamani isiyopungua sh,milioni 100 kilichofanyiwa uthamini kwa mthamini anayetambulika.
Masharti mengine ni kwamba washtakiwa hawatakiwi kutoka nje ya mkoa huo bila kibali cha mahakama.
Washtakiwa hao hawakuweza kutimiza masharti ya mahakama na walipelekwa mahabusu katika gereza kuu la karanga mjini Moshi.