Kaulimbiu iliyoiongoza Klabu ya Simba kuelekea kufuzu Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF dhidi ya wapinzani wao Al Masry “Hii Tunavuka” imezaa matunda na sasa si kusema tena “Hii Tunavuka” bali “Tumevuka.”
Kimsingi, Klabu ya Simba ilikuwa na wakati mgumu sana katika mechi hii licha ya ujasiri waliokuwa nao wachezaji, viongozi wa Simba, mashabiki na wadau wa soka nchini, lakini kazi haikuwa rahisi hata kidogo. Kivipi? Katika mechi ya ugenini dhidi ya Al Masry, Simba ilipoteza mechi hiyo kwa kukubali kipigo cha magoli mawili, bila wao kupata hata goli moja (2-0).
Hivyo, katika mechi ya Aprili 09, 2025 katika uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, Klabu ya Simba ilipaswa kupata ushindi wa magoli matatu katika dakika 90 au kupata ushindi wa magoli 2-0 ili baadae waweze kuingia katika hatua kwa ya penati. Lakini haya yote mawili hayakuwa rahisi hata kidogo. Yote yalikuwa magumu, asikudanganye mtu.
Meza ikapinduliwa, Klabu ya Simba ikafanikiwa kupata ushindi wa magoli mawili kufuatia wachezaji wao – Elie Mpanzu na Steven Mukwala kupachika magoli huku wapinzani wao wakikosa hata goli moja (2-0) katika dakika 90, hivyo kuwa sawa katika takwimu za jumla (2-2); Kwa maana ya kwamba kila timu katika uwanja wake wa nyumbani ilipata ushindi wa 2-0, hivyo, maamuzi ya kupiga penati yakachukua nafasi yake.
Katika hatua ya penati, Simba iliibuka na ushindi wa magoli manne dhidi ya moja (Simba 4 – Al Masry 1), huku mlindagoli, Moussa Camara akifaya kazi nzuri ya kudaka penati mbili, hali iliyorahisisha ushindi wa Klabu ya Simba.
Nini cha kujifunza hapa maishani?
Binafsi, nimepata somo kwamba katika maisha “Usikate tamaa” wengine wanakwenda mbali sana, wanasema “Mafuruku kukata tamaa.” Katika hali ya kawaida, Klabu ya Simba ilikuwa na wakati mgumu sana kama niliyoeleza hapo juu kufuzu Nusu Fainali lakini yote katika yote imefanikiwa kuingia Nusu Fainali na kuepukana na utani wa kuitwa “Mwakarobo” yaani watu wanaoishia Robo Fainali tu. Kufuzu Nusu Fainali ilikuwa ni jambo ambalo ni kiu na hamu kubwa kwa wachezaji, viongozi na mashabiki wa Klabu ya Simba.
Nataka kusema nini hapa? Tusikate tamaa. Kuna rafiki yangu moja anaitwa Shaban Kurwa James, katika harakati za kupeana hamasa za kupambana katika maisha, aliwahi kuniambia “Mtu yeyote ambaye anapumua yaani yuko hai, anaweza kutimiza ndoto zake, ni maiti/mtu mfu pekee ndiye asiyeweza kutimiza ndoto zake ili mradi uko hai, unaweza kutimiza ndoto na malengo yako.”
Kiukweli, si mara zote katika maisha mazingira yatakiwa rafiki au kukupa uhakika wa kufanikiwa katika mipango yako. Ni katika ugumu huo huo, njia ya kufanikiwa huwepo pia. Tusikate tamaa katika jambo lolote iwe ni katika elimu, biashara, ndoa, uwekezaji, malengo mbalimbali ya maisha na mengine kadha wa kadha, tusikate tamaa. Hili ndio nililojifunza katika mechi ya Aprili 09, 2025 kati ya Simba na Al Masry.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga.
Maoni: 0620 800 462.