
Wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Jimbo la Geita wameungana kwa nguvu kupinga kile wanachokiita “kesi ya kisiasa” dhidi ya Mwenyekiti wao, Tundu Lissu, aliyekamatwa Aprili 9, 2025, huko Mbinga – Ruvuma, kwa tuhuma za uhaini na kusambaza taarifa za uongo.
Katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Kata ya Nzera, Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Geita, Neema Steven Chozaile, amesema:
“Hatukubaliani na hatua ya kumweka ndani mtu ambaye anatetea haki za wananchi. Lissu alikamatwa kwa kutoa elimu ya uraia – si kwa kuhatarisha usalama wa nchi!”
Kwa mujibu wa taarifa, Lissu alikuwa akihamasisha wananchi kuhusu haki yao ya kupiga kura na umuhimu wa ushiriki katika demokrasia. Wafuasi wake wanadai kuwa tuhuma za uhaini ni njama ya kuzima sauti ya upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.
Lissu bado yupo rumande akisubiri kesi ya uhaini inayotarajiwa kusikilizwa tena Aprili 24, 2025. Kuhusu kesi ya kusambaza taarifa za uongo – tayari amekana mashtaka hayo mahakamani.
CHADEMA GEITA: “NO REFORM, NO ELECTION!”
Wanachama wa CHADEMA Geita wamesisitiza kuwa bado wanasimamia msimamo wao wa kitaifa wa “No Reform, No Election”, wakidai ni lazima kuwe na mageuzi ya kweli ya uchaguzi kabla ya kura ya mwaka huu.