Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeipongeza Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa kuzingatia maoni na ushauri unaotolewa na kamati hiyo ili kuhakikisha mchakato wa ajira unafanyika kwa ufanisi mkubwa na uwazi wa hali ya juu.
Akizungumza Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Madaba Mkoani Ruvuma Dkt. Joseph Kizito Mhagama, ametoa pongezi hizo Jijini Dodoma kwa niaba ya Kamati yake wakati wa ziara ya kikazi ya Kamati hiyo iliyolenga kutembelea na kujifunza utendaji kazi wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.
Dkt. Mhagama ametolea mfano maoni ambayo Kamati yake iliyatoa kuhusu usaili kufanyika katika ngazi za mikoa badala ya kuwalazimu waombaji kazi wote kufika Dodoma kumeleta matokeo chanya kwa waombaji kazi hao.
Vilevile, Dkt. Mhagama amezungumzia matumizi ya mfumo wa Ajira Portal kwa waombaji kazi kuondokana na dhana tofauti ya upendeleo wa kupata ajira katika Utumishi wa Umma.
“Mfumo wa Ajira Portal umeondoa dhana ya kuwepo kwa upendeleo kwa waombaji kazi, ninaamini wengi wamepata ajira serikalini pasipo kupitia kwa mtu yeyote,” amesema Mhe. Dkt. Mhagama.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu, ameishukuru Kamati hiyo kwa kutoa maoni na ushauri mara zote ambao kwa kiasi kikubwa umesaidia kutekeleza majukumu ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kikamilifu.
Aidha, Naibu Waziri Sangu amewaomba Wajumbe wa Kamati hiyo kuendelea kuwa Mabalozi wazuri wa Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma ili kuwahakikishia wananchi kuhusu uwazi wa namna ajira katika Utumishi wa Umma zinavyopatikana kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa na Sekretarieti hiyo wakati wa kuomba kazi.
Akielezea mafanikio baada ya kutumia mfumo wa Ajira Portal, Kaimu Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Mhandisi Samweli Tanguye amesema, kupitia mifumo wameweza kuajiri Rasilimaliwatu yenye uwezo wa kufanya kazi na kutoa matokeo chanya pamoja na kuondoa hoja za kuajiri kwa dhana ya upendeleo.