
Serikali ya Tanzania, kupitia Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe, imetangaza rasmi kuzuia kuingia nchini kwa mazao ya aina yoyote kutoka Afrika Kusini na Malawi kuanzia sasa hadi hapo itakapotolewa taarifa mpya. Hatua hiyo inakuja kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni changamoto za kibiashara zinazohatarisha maslahi ya wakulima na wafanyabiashara wa ndani.
Mbali na hilo, mizigo ya mazao, mbolea au bidhaa nyingine za kilimo zinazopitia Tanzania kuelekea Malawi nazo zimezuiliwa kupita, huku Serikali ikisema mazungumzo ya kidiplomasia yanaendelea chini ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
“Hatua hii inalenga kulinda masoko ya ndani dhidi ya ushindani usio wa haki na kuweka kipaumbele kwa wakulima wa Tanzania,” alisema Bashe.
Je, Vita ya Kibiashara Inakaribia?
Hatua hii, ingawa ni ya muda, inaleta hisia za mwanzo wa migogoro ya kibiashara (trade tension) kati ya Tanzania na majirani zake Malawi na Afrika Kusini. Kama mazungumzo hayatazaa matunda haraka, kuna uwezekano mkubwa wa kushuhudia hatua za kulipizana – mfano Malawi nayo kuzuia bidhaa kutoka Tanzania, au Afrika Kusini kuimarisha vizuizi kwa bidhaa za Tanzania.
Athari Kwa Tanzania: Wakulima wa ndani watanufaika kwa muda mfupi kwa kupata soko la ndani lisilo na ushindani wa bidhaa kutoka nje. Hata hivyo, bidhaa kama matunda na mazao ya kimkakati yaliyokuwa yanapita kwenda nchi hizo sasa yatakosa soko, jambo ambalo linaweza kuathiri mapato ya walaji na wakulima wa Tanzania wanaohusika na biashara ya nje.
Athari Kwa Malawi na Afrika Kusini: Malawi, ambayo hutegemea Tanzania kama njia ya kupitisha mazao kwenda sokoni, inaweza kukumbwa na changamoto kubwa za usafirishaji.