NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, wamefanikiwa kuzuia tani 14 za kemikali bashirifu zilizokuwa ziingizwe nchini kinyume cha sheria.
DCEA imefanikiwa zoezi hilo wakati wakifanya operesheni katika mikoa ya Dar es Salaam, Shinyanga, Tabora, Tanga, Songwe, Mbeya na Arusha ambapo pia wamefanikiwa kukamata pakti 10 za pipi zenye uzito wa gramu 174.77 zilizotengenezwa kwa kutumia bangi, kukamata kilogramu 4,568 za dawa mbalimbali za kulevya na kuteketeza ekari 178 za mashamba ya bangi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 24, 2025 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa DCEA Kamishna Jenerali Aretas Lyimo amesema mpaka sasa wanayashikiria magari saba, pikipiki tano na bajaji moja vilivyohusika kwenye uhalifu huo.
Amesema jumla ya watuhumiwa 35 wamekatwa na taratibu za kisheria zinaendelea dhidi yao.
Aidha Kamishna Lyimo amesema kwa kushirikiana na Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Duniani (INCB) na mamlaka nyingine za udhibiti, DCEA ilibaini na kuzuia kilogramu 4,000 za kemikali aina ya 1-Boc-4-piperidone na kilogramu 10,000 za kemikali aina ya Acetic anhydride zilizokuwa ziingizwe nchini kutokea bara la Asia bila kuwa na vielelezo vinavyoonesha matumizi ya kemikali hizo.
“Endapo kemikali hizi zingeingizwa nchini na kuchepushwa zingeweza kutumika kutengeneza dawa za kulevya aina ya fentanyl na heroin”. Amesema
Amesema Mathalani, kilogramu 4,000 za kemikali aina ya 1-Boc-4-piperidone zinaweza kutengeneza kilogramu 8,000 za dawa za kulevya aina ya fentanyl.
Pamoja na hayo amesema kuwa matumizi ya kiasi hicho cha dawa za fentanyl ambazo zingezalishwa zingeweza kusababisha vifo kwa watumiaji bilioni nne (4) ikizingatiwa kwamba, kilogramu moja (1) ya dawa hizo inaweza kusababisha vifo kwa watu 500,000 kutegemea na uzito, afya, na historia ya mtumiaji (miligramu mbili (2) inaweza kusababisha kifo kwa mtu mmoja).