Na Mwandishi Wetu.
KATIKA jitihada za kuongeza uhifadhi wa mazingira katika wilaya za Chemba na Kondoa mkoani Dodoma, shirika lisilo la kiserikali (NGO) la limetoa msaada wa mizinga ya kisasa ya nyuki 70 yenye thamani ya Shilingi milioni saba kwa wafugaji wa nyuki.
Msaada huu si tu utaongeza uzalishaji wa asali katika vijiji viwili vya Gwandi (Chemba) na Sambwa (Kondoa), bali pia utaongeza kipato cha wakulima na wakati huo huo kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Sambamba na msaada huo shirika hilo pia limejengea uwezo wafugaji wa nyuki katika wilaya hizo mbili kwa kutoa mafunzo kwa mafundi wa mitaa kuhusu utengenezaji wa mizinga ya kisasa ya nyuki, ili kuwawezesha kuongeza uzalishaji wa asali na kuboresha maisha yao kupitia shughuli za kiuchumi.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya mizinga hiyo katika kijiji cha Gwandi, wilayani Chemba hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Inades-Formation Tanzania (IFTz), Mbarwa Kivuyo amesema msaada huo kwa wakulima unalenga kuboresha maisha ya wafugaji wa nyuki na kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa sehemu ya ulinzi na uhifadhi wa mazingira.
Kivuyo amesema kila kijiji kitapokea mizinga 35 kutokana na juhudi walizozionyesha katika uhifadhi wa mazingira kwa kulinda misitu na vyanzo vya maji.
“Kupitia ufugaji wa nyuki, miti itahifadhiwa na kulindwa na hii itasaidia kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika wilaya hizi mbili zenye ukame.” amesisitiza Kivuyo.
Kwa mujibu wa Kivuyo, kwa kushirikiana na Bread for the World (BftW), IFTz inatekeleza miradi mbalimbali ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi katika wilaya hizo mbili na pia wanapanga kutoa mafunzo kwa mafundi cherehani wa mitaani ili kutengeneza mavazi ya kujikinga kwa wafugaji wa nyuki wakati wa uvunaji wa asali.
“Tunahitaji kuona wafugaji wa nyuki katika vijiji vya Chemba na Kondoa wanakuwa mabingwa wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi na pia kuwa na vifaa vya kisasa wakati wa kuvuna asali. ” Ameongeza.
Ripoti zinaonesha kuwa uvunaji wa asali kwa njia za jadi huharibu misitu kwani huhusisha kukata miti kwa ajili ya kutengeneza mizinga ya kienyeji ambayo huvunjwa kila msimu wa mavuno.
Nae, Afisa wa Mazingira wa Wilaya ya Chemba, Mohamed Semdoe amesema kuwa utekelezaji wa miradi ya IFTz katika wilaya hiyo umeleta mafanikio makubwa kiasi cha halmashauri kufikiria kuwekeza katika kiwanda cha kuchakata asali kijijini hapo.
Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza thamani ya bidhaa ya asali, kuwawezesha wafugaji kuongeza kipato na hivyo kuimarisha usalama wa chakula kwa wakulima, huku akibainisha kuwa ni njia mojawapo ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi kupitia ufugaji wa nyuki.
Katibu wa kikundi cha ufugaji nyuki cha Juhudi, Salmin Dosa amesema msaada wa IFTz utaongeza uzalishaji wa asali kutoka wastani wa lita 1 hadi 3 kwa mzinga wa kienyeji hadi kufikia lita 18 kwa mzinga wa kisasa.
“Msaada huu pia utasaidia sana kuhifadhi mazingira ya kijiji chetu kwa manufaa ya vizazi vijavyo,” amesema.