Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
NAIBU Waziri wa afya DKt Godwin Mollel ameitaka hospitali ya Rufani ya Kanda ya Benjamin Mkapa (BMH),kutoka katika hatua ya kanda na kuelekea kuwa hospitali ya Taifa,kutokana na utoaji tiba za magonjwa mbalimbali ambayo awali matibabu hayo yalikuwa yakipatikana nje ya nchi.
Dkt Mollel ameyazungumza hayo wakati akifunga mafunzo ya huduma za dharura yaliyoanza Mei 12 hadi 16 2025 jijini Dodoma.
Amesema BMH imekuwa ikitoa huduma kubwa za matibabu kama vile upasuaji wa ubongo kwa kutumia sauti ya mawimbi pamoja na upasuaji wa moyo kwa njia ya matundu,ambapo teknolojia hizo awali zilipatikana nje ya nchi.
Amesema asilimia 97 ya wagonjwa waliokuwa wakienda nje kutibiwa kwa magonjwa mbalimbali hivi sasa wanatibiwa hapa nchini ikiwemo katika hospitali hiyo ya BMH.
Amefafanua kuwa mabadiliko hayo,yanatokana na uwekezaji unaofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na kupelekea taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kufanya mabadiliko hayo.
“Nampongeza Profesa Abel Makubi kwa kazi nzuri anayoifanya nanyie hospitali ya Mirembe igeni mfano huu wa kufanya bunifu mbalimbali ili kuboresha hospitality hiyo,”amesema Dkt Mollel.
Naye Mkurugenzi wa BMH Profesa Abel Makubi aliishkuru Seriiali kutokana na uwekezaji inayofanya katika sekta ya afya na kupelekea kufanyika Kwa mabadiliko hayo katika maeneo mbalimbali.
Profesa Makubi pia amewataka waliopata mafunzo hayo kwenda kuyatumia kwa vitendo ili waweze kutoa huduma za kitabibu kwa weredi Kwa upande wa dharula.
Naye , mwakilishi wa Waziri wa Afya wa Uturuki, Dkt. Mustapher Kucuk, amesema programu hii inaonyesha mahusiano makubwa yaliopo kati ya Tanzania na Uturuki.
“Programu hii iliyotuleta hapa pamoja ni uthibitisho wa ushirikiano imara tulionao kati ya Serikali ya Tanzania na Uturuki,” amesema Dkt Kucuk.
Mafunzo hayo yameratibiwa na Idara ya Magonjwa ya Dharura ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) na kuwezeshwa na Shirika la Maendeleo la Uturuki (TIKA) yamewaleta pamoja washiriki 32 kutoka sekta mbalimbali.