Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Edward Mpogolo (wa tatu kushoto) akiwa na Meneja Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Julius Mnganga (wa pili kulia) wakiwa na mfano wa cheki ya shilingi milioni 735 ziliztolewa kwa vikundi 25 vya wajasiriamali waliokidhi vigezo vya kupata mikopo shirikishi itokanayo na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri inayotolewa na CRDB Bank Foundation na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala. Wengine katika picha ni Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Mheshimiwa Omary Kumbilamoto (katikati), Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya (wa tatu kushoto). Wengine ni Meneja wa Tawi la Benki ya CRDB Gongolamboto, Wemaeli Msechu (wa kwanza kushoto), Meneja wa Tawi la Benki ya CRDB Ilala, Mariamu Mrema (wa pili kushoto) na Mchambuzi wa Ruzuku wa CRDB Bank Foundation, Frank Kahatano (wa kwanza kulia).
===== ===== =====
Dar es Salaam: Baada ya kukamilisha maandalizi yote muhimu ya kuwawezesha wajasiriamali wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, Taasisi ya CRDB Bank Foundation kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imezingua utoaji wa mikopo itokanayo na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.
Uzinduzi huo ulioongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Edward Mpogolo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila, ulifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita umekuja baada ya kukamilika kwa mchakato wa kuwashirikisha wananchi kwa kuwapa mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha.

“Miaka minne iliyopita, Ilala ilikuwa inakusanya shilingi bilioni 61 kwa mwaka lakini sasa mapato yamepanda mpaka shilingi bilioni 138 hivyo fedha zinazotengwa kwa ajili ya wajasiriamali ni nyingi na zitaendelea kuongezeka kila mwaka.
Tunashirikiana na CRDB Bank Foundation kuwafikia wananchi wengi kadri iwezekanavyo. Niwaombe wajasiriamali walio tayari, jitokezeni ili kunufaika na mikopo hii,” amesema Mheshimiwa Mpogolo.
Akieleza utayari uliopo, Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya amesema jumla ya shilingi bilioni 18 zipo tayari kukopeshwa hivyo akawataka wananchikujitokeza akibainisha kuwa kuna vikundi 945 vilivyojitokeza mpaka sasa.
“Asilimia 4 ya fedha hizi ni kwa ajili ya wanawake na asilimia 4 nyingine zimeelekezwa kwa vijana na asilimia mbili zilizobaki ni za watu wenye ulemavu. Wanawake mmepewa nafasi kubwa zaidi kwani ndani yenu kuna vijana na watu wenye ulemavu pia hivyo ukichambua kwa umakini unaweza kukuta ninyi mnapata mpaka asilimia 80 ya kiasi chote kilichopo hivyo niwasihi muichaangamkie fursa hii iliyo mbele yenu,” amesema Mabelya.
Hata hivyo, walengwa wa mikopo hiyo walikumbushwa umuhimu wa kutimiza wajibu wao kwa kueepuka udanganyifu wanapotoa taarifa zao, waunde vikundi kwa nia halisi ya ujasiriamali, kusajili biashara zao na waombe mkopo kwa biashara wanazozimiliki.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Mwambapa, Meneja Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Julius Mnganga amesema mpaka sasa wameshavifikia vikundi 120 ambavyo vimewasilisha maombi ya mikopo yenye thamani ya jumla kiasi cha shilingi bilioni 3.
Hata hivyo, Mnganga amesema baada ya kuvitembelea vikundi hivyo pamoja na wanachama wake wamekuta vikundi 25 ndivyo vinakidhi vigezo vya kunufaika na mikopo hiyo kwa sasa.
“Vikundi hivi 25 vimeleta maombi yenye thamani ya shilingi milioni 735. Tunaendelea kutoa elimu ili kuviwezesha vikundi vyote vilivyoleta maombi ili vikamilishe vigezo vinavyohitajika kunufaika na mikopo hii nafuu. Nitumie fursa hii kuwakaribisha wajasiriamali wengine ndani ya Manispaa ya Ilala kuja kuomba uwezeshaji huu ili wakuze biashara zao,” amesema Mnganga.
Katika vikundi 120 vilivyojitokeza, Mnganga amesema 75 ni vya wanawake, vikundi 43 vya vijana na vikundi viwili ni vya watu wenye ulemavu. Kuhusu vikundi 20 vilivyokidhi vigezo, amesema vikundi 13 vya vijana, vimeomba jumla ya shilingi milioni 532 huku vikundi 11 vya wanawake vikihitaji shilingi milioni 198 na kikundi kimoja cha watu wenye ulemavu shilingi milioni 5.
Taasisi ya CRDB Bank Foundation imeahidi kuendelea kushirikiana na maafisa maendeleo wa Manispaa ya Ilala pamoja na viongozi wa vikundi husika kuwasaidia wanachama wao kurekebisha kasoro zilizopo ili wote wenye nia njema wanufaike na mikopo hii.
“Jambo muhimu kulizingatia muda wote ni kurejesha fedha hizi kwa wakati. Wote mtakaopewa mikopo hii msisahau kuirejesha kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa tunatoa nafasi kwa wengine nao kukopa,” amesisitiza Mnganga.