MENEJA wa Mfuko wa Self MF Kanda ya Kati Dodoma na Singida Aristid Tesha amesema kuwa kwa sasa mfuko huo umeanzisha bidhaa mpya ambapo wanatoa mikopo kwa wajasiriamali wanaojihusisha na Nishati mbadala,Nishati safi wanajikita katika kuuza bidhaa za gesi na vifaa vyake.
Aliongeza kuwa wanaangalia kwa waliojikita kwenye mambo ya vifaa vya umeme wanazitumia kama Nishati mbadala.
Alisema hiyo yote ni nia ya serikali ya kumfanya Mtanzania apunguze matumizi ya mkaa,kuni katika eneo linalomzunguka.
“Hawa wanaofanya Nishati mbadala tumewalenga na tunawapa mkopo wenye riba nafuu ili waweze kupanua wigo kufanya shughuli zao na kuweza kuwafikia wananchi,” alieleza.
Alifafanua kuwa kwenye Nishati mbadala wamejikita kwa wanaosambaza sola za umeme waliopo vijijini na mijini wanaowauzia wananchi kwa bei nafuu.
Aidha akizungumzia mikopo ya watumishi wa Umma alisema kuwa wanatoa mikopo kwa watumishi kupitia mishahara yao ambapo huduma ya mikopo hiyo inapatikana katika matawi yaliyopo mikoa 12.
Hata aliwahimiza wananchi kutembelea banda la Self MF ili waweze kupata maelezo ya huduma mbalimbali zinazotolewa na mfuko huo.
Naye Meneja Rasilimaliwatu na Utawala Johari Magara alieleza kuwa lengo kuu la kushiriki maadhimisho hayo ni kuwapa huduma wananchi ya kuwapa taarifa ya huduma za mikopo zinatolewa na mfuko huo.
Alieleza kuwa mfuko wa self MF ulianza rasmi 2014 ambapo lengo kuu ni kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwapatia mikopo yenye unafaa.
“Mikopo ya Self MF ya aina mbalimbali ikiwemo mikopo ya watumishi wa Umma, wafanyabisahara, wajasiriamali wadogo na wa kati, mikopo ya wakulima, mkopo wa wazabuni pamoja na Nishati safi,”alisema.
Alieleza kuwa mbali na mikopo hiyo pia mfuko huo unatoa mkopo wa bima za gari,nyumba, za wizi na nyingine zote.