Na Pamela Mollel, Kilimanjaro
Wadau wa utalii hapa Tanzania wameaswa kubuni mazao mbalimbali ya utalii ambapo mazao hayo yataweza kutangaza fursa mbalimbali zilizopo
Hayo yameelezwa na mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu wakati akizindua kampeni ya twenzetu kileleni msimu wa 5 ambayo inaandaliwa na kampuni kubwa ya utalii ya Zara tours iliopo Moshi
Nurdin alisema kuwa wadau wa utalii wanapokuwa wanabuni mazao au kampeni mbalimbali za utalii inaweza kuruhusu fursa za kitalii kuweza kutafahamika na hivyo kufanya hata mapato ya utalii kuongezeka
“Kampuni ya Zara imeonesha ufanisi mkubwa sana wa kubuni na Kisha kutekeleza kampeni hii ambayo sasa ni awamu ya Tano kwa mwaka huu lakini pia kila mara inakusanya watu wengi,niwatake makampuni mengine sasa kuiga hili na Kisha kutuletea kitu kipya kabisa”aliongeza
Wakati huo huo aliwataka hata wadau utalii kwa mara nyingine kuhakikisha kuwa wanawekeza zaidi kwenye ujenzi wa nyumba za wageni kwa kuwa sekta ya utalii imekuwa kwa kiwango kikubwa
“Watalii ni wengi kutokana na kampeni ya MaMa Samia sasa wageni wengine wanakuja kujionea vivutio vya utalii lakini wanalala mkoa wa Arusha Nathani hii ni fursa kubwa sasa kuwekeza.
“Tukiangalia hapa mdau wa utalii kama Zara Tours ameweza kutuwakilisha vyema na wageni wanakuja hapa wanashukia hapa sasa ni wakati hata wa makampuni mengine basi waweze kuiga hili ili fursa zije lakini pia hata kumuunga mkono Raisi Samia Suluhu Hassan juu ya kampeni ya Royal Tours “
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Zara Tanzania Adventure,Bi Zainab Ansel alisema kuwa anamshukuru sana Raisi wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwa naye ameweza kutangaza nchi sana na hivyo kuruhusu wageni wengi Kuja nchini
Bi Zainab alisema kuwa watalii wapo,lakini kupitia kampuni yake ya Zara wanatarajia kuhamasisha watu zaidi ya 200 kuweza kupanda mlima wa kilimanjaro
“Tunahamasisha watanzania waweze kupanda mlima kilimanjaro maana hata juzi tu hapa mlima kilimanjaro ulipata tuzo,na kupitia kampeni hii pia na sisi tutangaza utalii wetu ipasavyo”aliongeza
Kamapeni hiyo ya twenzetu kileleni inatarajiwa kufanyika mwezi December mwaka huu ikiwa ni maalumu kwa kukuza utalii wa ndani sanjari na kuadhimisha miaka 64 ya uhuru wa nchi ya Tanzania.